RAIS SAMIA AKUTANA NA MISHENI YA AUEOM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi kutoka Umoja wa Afrika (AUEOM), ukiongozwa na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana na Kiongozi wa Misheni hiyo, Mhe. Mokgweetsi Masisi, Ikulu ndogo Tunguu, Zanzibar.
Kwenye mazungumzo yao, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameishukuru AUEOM kwa kukubali wito wa kuungana na waangalizi wengine wa Uchaguzi wa Kimataifa katika kuangalia Uchaguzi Mkuu wa Tanzania 2025.
Mhe. Rais Samia amewakaribisha na kuwatakia majukumu mema na kuwaahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwapa ushirikiano katika kipindi chote wawapo nchini na kueleza kuwa Tanzania inathamini mchango wa Misheni za Kimataifa katika kuchangia ukuaji wa demokrasia barani Afrika.
Kwa upande wake, Mhe. Masisi ameipongeza Tanzania kwa kuilinda amani katika kipindi hiki na kushukuru kwa ushiriki wa AUEOM katika uchaguzi wa 2025. Aidha, ameishukuru Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuratibu Misheni hiyo na wadau wa uchaguzi. Amesisitiza kuwa AUEOM inaenda kufanya kazi yake kwa weledi na ustadi kwa kufuata taratibu, sheria na miongozi ya Umoja wa Afrika ili kuendelea kulinda demokrasia Afrika.
Pamoja na hayo, Misheni hiyo imeridhishwa na utekelezwaji wa mapendekezo waliyoyatoa kwenye ripoti yao ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.
Ujumbe wa Misheni ya AUEOM utakutana pia na vyama vya siasa nchini Tanzania vinavyogombea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.







