RC CHALAMILA: WANANCHI DAR ES SALAAM JITOKEZENI KWA WINGI KUPIGA KURA, MKOA UKO SALAMA
Na Neema Mpaka - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila amewataka wananchi wakazi wa Mkoa huo kupuuza taarifa za uzushi zinazotolewa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii kuwa uchaguzi utakua na vurugu badala yake wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwani Mkoa uko Salama wakati wote kabla ya uchaguzi,wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi
Akizungumza leo octoba 27 2025 Jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari RC Chalamila amesema Mkoa wa dare es salaam una wapiga kura zaidi milioni nne na kwamba tayari tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imeshakamilisha miundombinu kwa ajili ya wananchi kupigia kura
Aidha amewataka wananchi kujitokeza kupiga kura bila kuhofia usalama wao kwani vyombo vya ulinzi vimejipanga vizuri kuimarisha amani
"Navionya vikundi vinavyotishia kuvuruga amani wakati wa uchaguzi kupitia mitandao ya kijamii kuwa vyombo vya dola viko macho vitachukua hatua dhidi ya mtu atakayebainika kufanya au kutaka kuleta vurugu na hivyo naomba wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya dola endapo kuna viashiria vya vurugu" Amesema Chalamila.
Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kila mwananchi anapata nafasi ya kutumia haki yake ya kikatiba ya kupiga kura bila hofu wala vurugu kwakua Serikali inatambua kuwa suala hilo ni haki ya kikatiba.
Pamoja na mambo mengine Chalamila amevitaka vyombo vya habari kufanya kazi kwa weledi bila kufanya upotoshaji kwani vyombo vya habari ni muhimili muhimu ambao ni kiunganishi kati ya wananchi na Serikali yao.
Kadhalika RC Chalamila amewataka viongozi kuanzia ngazi ya serikali ya mitaa kulinda miundombinu ya Serikali ikiwemo ya umeme, barabara za mwendokasi ambapo amesisitiza barabara hizo kutotumiwa na vyombo vingine vya usafiri.




