TAIFA LAKUNJA JAMVI: MACHO YOTE SASA OKTOBA 29
Na Mwandishi Wetu - Kuelekea kilele cha mchakato wa kidemokrasia nchini, Watanzania wako katika siku za mwisho za maandalizi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu unaosubiriwa kwa hamu, ambao utafanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025. Jumla ya vyama 17 vya siasa vinakamilisha rasmi mikutano na maandamano yao ya kampeni, yaliyotawaliwa na ahadi za maendeleo, huku nchi ikiingia katika kipindi cha utulivu wa mwisho kabla ya kura kupigwa.
Kampeni za Amani na Ukomavu wa Demokrasia
Msimu wa kampeni za mwaka huu unatajwa na wachambuzi wengi wa siasa kuwa mojawapo ya misimu iliyokuwa tulivu na yenye ukomavu zaidi katika historia ya hivi karibuni ya taifa. Vyama vyote, vikiwemo vile vikubwa na vidogo, vimefanya mikutano yake kwa kuzingatia kwa kiasi kikubwa sheria na Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zilizowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe, alipongeza mwenendo mzima.
"Tunaipongeza jamii nzima ya Watanzania na viongozi wa vyama 17 kwa kukamilisha kampeni bila ya matukio makubwa (vituko) yanayowezahatarisha amani yetu. Hii inaonyesha kwamba maslahi ya taifa na amani yetu ni kipaumbele kwa kila Mtanzania," alisema.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa TBN, kesho ni wakati wa wananchi kufanya maamuzi yao ya mwisho na kujitokeza kwa wingi.
"Tunawahimiza Watanzania wote waliojiandikisha kutumia Siku hii ya Mapumziko (Oktoba 29) kama fursa ya kipekee ya kufanya mabadiliko wanayoyahitaji katika uongozi," alisema Kiongozi huyo. "Kila kura ni muhimu. Kura yako ndiyo itakayochagua viongozi watakaobeba matumaini makubwa ya taifa letu katika miaka mitano ijayo. Jitoeni na mpige kura kwa kuzingatia kikamilifu sheria zote za uchaguzi."
Katika taarifa yake alisema kwamba TBN inasisitiza amani kama msingi mkuu wa maendeleo. Wananchi wanatakiwa kutunza utulivu kabla, wakati, na baada ya upigaji kura. Tume ya Uchaguzi inapaswa kuheshimiwa, na migogoro yoyote ishughulikiwe kwa njia za kisheria na amani.
Akizungumzia hali baada ya uchaguzi Msimbe alisema TBN inasisitiza amani, umoja, na mshikamano vinapaswa kupewa kipaumbele ili kuendeleza gurudumu la uchumi na ustawi wa jamii.
"Tuweke tofauti za kisiasa kando baada ya uchaguzi na kuanza safari mpya ya kuijenga Tanzania yenye ustawi. Uchaguzi bora ni ule unaojenga maendeleo na matumaini," alimalizia Kiongozi wa TBN.



