TBN YAHIMIZA WANANCHI KUJITOKEZA KUPIGA KURA KESHO OKTOBA 29, 2025
Dar es Salaam, Oktoba 28, 2025 - Mtandao wa Wablogu Tanzania — Tanzania Bloggers Network (TBN) umetoa pongezi kwa Watanzania wote, wagombea wa vyama vya siasa, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), na wadau mbalimbali kwa kukamilisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 katika mazingira ya amani na utulivu.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam, TBN imesema kipindi chote cha kampeni kimekuwa cha utulivu na heshima, bila matukio makubwa yaliyoweza kuhatarisha amani na umoja wa taifa.
“TBN inatambua na kupongeza juhudi kubwa zilizofanywa na washiriki wote katika kipindi chote cha kampeni, ambapo hakukuwa na matukio makubwa ambayo yangehatarisha amani na umoja wa taifa letu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, mtandao huo umesifu namna washiriki wa uchaguzi walivyofuata sheria, kanuni, na taratibu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi, ikiwemo Kanuni za Maadili ya Uchaguzi, hatua ambayo imesaidia kudumisha uchaguzi huru, wa haki na wa amani.
“Amani yetu ni urithi na hazina kubwa. Mwenendo wa kampeni za mwaka huu umethibitisha kwamba Watanzania wanaiweka amani na maslahi ya taifa mbele ya tofauti za kisiasa,” amesema Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe.
TBN pia imewahimiza Watanzania wote wenye sifa za kupiga kura kujitokeza kwa wingi kesho, Jumatano Oktoba 29, 2025 siku ambayo imetangazwa rasmi kuwa siku ya mapumziko ili kutekeleza haki yao ya kidemokrasia.
“Kura yako ni sauti yako ya kufanya mabadiliko na kuchagua mustakabali wa taifa letu. Tuitumie siku hii kama fursa ya kuweka msingi wa maendeleo endelevu,” imesisitiza taarifa hiyo.
TBN imewakumbusha wananchi kuendelea kudumisha amani na umoja wakati wa zoezi la kupiga kura na kusubiri matokeo kwa utulivu, huku ikiwatakia Watanzania wote uchaguzi mwema na wenye mafanikio.
Mwisho wa taarifa umeeleza:
“Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki amani yetu.”




