UMOJA WA ASASI ZA KIRAIA WA SHULE SALAMA WATOA WITO WA KUWALINDA WATOTO KABLA NA BAADA YA UCHAGUZI MKUU 2025
Miongoni mwa wanachama wa Umoja huo ni HakiElimu, Save the Children, Msichana Initiative, TAMWA, WILDAF na CAMFED wakiongea katika mkutano na waandishi wa habari juu ya wito wa dharura kwa wadau wote nchini kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 mapema leo oktoba 1,2025 jijini dar es salaam.
Mratibu wa program ya My Legacy, Bi Amina Ally akisoma tamko kwa niaba ya Umoja huo ulio na zaidi ya asasi 20 zinazofanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 katika mkutano na waandishi wa habari mapema leo oktoba 1.2025 jijini dar es salaam.
Mratibu wa program, utafiti na ufatiliaji kutoka Jukwaa la Utu wa mtoto (CDF), Bi. Irene Ernest akizungumza katika mkutano huo na waandishi wa habari juu ya wito wa dharura kwa wadau wote nchini kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 mapema leo oktoba 1,2025 jijini dar es salaam
Dar es Salaam - Umoja wa Kitaifa wa Asasi za Kiraia wa Shule Salama (NSSC) umetangaza wito wa dharura kwa wadau wote nchini kuhakikisha ulinzi na usalama wa watoto kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akisoma tamko kwa niaba ya Umoja huo ulio na zaidi ya asasi 20 zinazofanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar, Mratibu wa program ya My Legacy, Bi. Amina Ally amesema kuwa kipindi cha uchaguzi kimekuwa kikiweka watoto kwenye hatari kubwa ya ukatili, kutelekezwa na hata kutumika vibaya katika shughuli za kisiasa.
Kwa mujibu wa sheria, mtoto ni yeyote mwenye umri chini ya miaka 18, na hivyo haruhusiwi kushiriki uchaguzi kwa namna yoyote. Hata hivyo historia inaonesha kuwa watoto mara nyingi hukumbwa na madhila katika kipindi cha uchaguzi, hususan watoto wenye ulemavu na hasa wenye ualbino ambao huwekwa hatarini kutokana na imani potofu.
Katika wito huo, Umoja huo umetoa mapendekezo mahsusi kwa makundi mbalimbali:
Mashirika ya kiraia (AZAKI/NGOs): kuendelea kutoa elimu ya uraia inayojumuisha ulinzi wa haki za watoto, kuripoti na kuhifadhi kumbukumbu za ukiukwaji, na kutoa msaada wa kisaikolojia kwa watoto wanaoathirika.
Vyombo vya habari: kuhakikisha sauti za watoto zinasikika, kuepuka lugha za chuki, kuripoti kwa maadili, na kuelimisha jamii kuhusu madhara ya kuhusisha watoto katika kampeni za kisiasa.
Vyama vya siasa na wagombea: kuweka kipaumbele kwenye haki na ustawi wa watoto katika ilani na kampeni zao, na kuacha mara moja utaratibu wa kuwatumia watoto kwenye mikutano ya kampeni.
Wazazi na jamii: kuhakikisha watoto wako salama karibu na vituo vya kupigia kura na mikusanyiko ya kisiasa, na kuwawajibisha wanasiasa kuhusu mipango yao ya kulinda watoto.
Serikali na vyombo vyake kuchukua hatua mapema kulinda watoto katika maeneo ya mikusanyiko ya kisiasa na kujibu kwa haraka matukio ya ukiukwaji dhidi ya watoto.
“Mtoto hana nafasi kisheria kwenye uchaguzi mkuu—iwe kupiga kura au kugombea. Hivyo hatutarajii kuona watoto wakihusishwa katika kampeni au mikutano ya kisiasa,” alisisitiza Bi Amina.
Aidha Umoja huo umehitimisha kwa kuwataka Watanzania wote kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa alama ya heshima kwa haki za watoto, ukiwapa nafasi ya kukua katika mazingira ya amani na usalama.
Miongoni mwa wanachama wa Umoja huu ni Kaya Foundation, HakiElimu, Save the Children, Msichana Initiative, TAMWA, WILDAF, Shule Direct, CAMFED na mashirika mengine.






