NSSF YASISITIZA WANANCHI KUJIUNGA NA MPANGO WAO MAALUMU WA HIFADHI SCHEME
Na Woinde Shizza , Arusha - Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kujiunga na mpango wao maalumu wa Hifadhi Scheme kupitia kampeni yao ya Staa wa Mchezo Paka Rangi, unaolenga kuandikisha na kuwakumbusha wanachama kulipia michango yao kwa wakati ili staa iendelee kung’ara.
Hifadhi scheme inalenga wananchi waliojiari wenyewe ikiwemo wajasiriamali wadogo, wakulima, wafugaji, mama lishe nk.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho ya Vyama vya Ushirika Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Arusha, Afisa Matekelezo wa NSSF Mkoa wa Arusha, Festo Mwakahesya, aliwataka wafanyakazi wa sekta rasmi na waliojiajiri kujitokeza kwa wingi kujiunga na mfuko huo.
“Tunawaomba wananchi, hasa wajasiriamali wadogo, wafanyabiashara, na hata walioajiriwa, wachangamkie fursa hii ambayo itakua msaada mkubwa pale mtu anapopatwa na majanga kama uzee, kifo, ulemavu nk alisema Mwakahesya.
Kwa upande wake, Afisa Matekelezo wa mfuko huo wa Hifadhi ya Jamii, Marietha Ngoma, alisema masharti ya kujiunga na Hifadhi Scheme kwa waliojiajiri ni rahisi, ambapo umri wa mwanachama unaanzia miaka 15 na ukomo wa kujiunga ni miaka 70.
Alitaja mafao yanayotolewa kupitia scheme hiyo kuwa ni pamoja na Mafao ya uzazi, Mafao ya matibabu,Mafao ya ulemavu,Mafao ya Pensheni ya uzee pamoja na Mafao ya msaada wa mazishi
Ngoma alibainisha kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupitia NSSF kuhakikisha kila Mtanzania anapata kinga ya hifadhi ya jamii na kuondoa dhana kwamba mafao hayo ni kwa ajili ya wafanyakazi wa sekta rasmi pekee.
Aidha amesisitiza kuwa Hifadhi Scheme ni kwa kila Mtanzania, ikiwa ni ngao ya usalama wa maisha ya sasa na ya baadaye.






