Breaking News

CUF YAPINGA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU, YAITAKA SERIKALI YA MPITO NA UCHUNGUZI WA MAUAJI.

Dar es salaam - Chama cha Wananchi CUF kimetangaza rasmi kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikidai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru, haki, wala wa kuaminika.

Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, amesema matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, yaliyompa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ushindi wa asilimia tisini na saba nukta sita sita ya kura, hayawakilishi maamuzi ya wananchi.

Profesa Lipumba amesema ni jambo lisilo la kawaida kuona ushindi wa kiwango hicho ukitangazwa wakati intaneti imefungwa kwa siku nne, vyombo vya habari vimedhibitiwa, na wananchi wanaishi kwa hofu.

“Uchaguzi huu haukuwa huru, haukuwa wa haki, na haukuwa wa kuaminika. Huu ni ubakwaji wa demokrasia,” amesema Profesa Lipumba.

CUF imesema mamia ya wananchi wamepoteza maisha wakati na baada ya uchaguzi.

Gazeti la The Guardian la Uingereza linaripoti vifo vya watu takribani 700, huku shirika la AFP likikadiria kuwa kati ya watu 500 hadi 800 wameuawa.

Mashirika mengine, kama Amnesty International, yameripoti vifo vya takribani 100, na Umoja wa Mataifa umethibitisha vifo visivyopungua kumi.

CUF inaitaka Serikali kuunda Tume Huru ya Uchunguzi inayoongozwa na jaji anayeaminika kuchunguza mauaji hayo na kuwawajibisha wahusika.

Chama hicho pia kimelalamikia kasoro nyingi katika mchakato wa uchaguzi, ikiwemo kura kupigwa kabla ya siku ya uchaguzi, mawakala wa upinzani kuzuiwa vituoni, na matokeo kutangazwa bila kuhesabiwa katika vituo husika.

CUF imesema wagombea wake waliokuwa na ushawishi mkubwa hawakutangazwa kushinda hata jimbo moja.

Wakati huo huo, Ujumbe wa Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC umesema uchaguzi wa Tanzania haukukidhi viwango vya uchaguzi huru na wa haki.

Ripoti yao imeeleza kuwa kulikuwa na ukandamizaji wa wapinzani, ukosefu wa uhuru wa vyombo vya habari, na matumizi ya nguvu za dola.

CUF sasa inataka kuundwa kwa Serikali ya Mpito itakayosimamia mabadiliko ya kisiasa, ikiwemo upatikanaji wa Katiba Mpya, mageuzi ya Tume ya Uchaguzi, na uhuru wa vyombo vya habari.

Pia, chama hicho kimetoa wito wa kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa wakiwemo Tundu Lissu, na kimewataka Watanzania kufanya ibada maalum ya kitaifa tarehe kumi Novemba kuwaombea waliopoteza maisha wakati wa uchaguzi.

Profesa Lipumba amesema, “CUF itaendelea kusimama upande wa wananchi, kutetea haki, demokrasia, na uhalali wa maamuzi ya Watanzania. Haki sawa kwa wote.”