Breaking News

KUTOKA MACHUNGU HADI UPENDO: WATANZANIA WAOMBA KURUDI KWENYE MAADILI BORA

Vurugu zilizotokea nchini hivi karibuni zimeacha majeraha, lakini pia zimechochea wito wa kitaifa wa kurejea kwenye misingi ya Utanzania—Maadili Bora, Upendo, na Mashauriano katika kutatua migogoro. 

Wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo walipohojiwa walisisitiza kwamba vurugu si utamaduni wetu, na kwamba njia ya kutafuta haki lazima iwe ya hekima, busara, na kuheshimu utu.

Siraji Ali Likwati, Mwenyekiti wa Bodaboda katika maeneo ya Kimara Matangini, Michungwani, na King'ongo, anaeleza kwa msisitizo mkubwa jinsi vurugu zinavyowaathiri hata wasiohusika.

 "Kama unataka haki basi haki fanya kwa namna haki inavyotakiwa kutakwa. Kilichofanyika hapa kwetu sio kutaka haki kwa sababu unakuta duka la mangi hana ushawishi wa siasa wa aina yoyote, yeye yupo na maisha yake anaendesha kwa biashara zake, lakini watu wanakuja wanavunja, wanachukua mali zake. Hiyo inakuwa mbaya zaidi."  

Anasema kama wananchi wengine waliohojiwa wanavyosema kwamba kuna namna ya kupeleka hoja lakini si kwa namna ya uporaji na kupeleka maumivu kwa nina la kutafuta haki.

Pia alisema kuna wajibu wa wananchi kusikiliza viongozi waliokuwapo kwa mujibu wa katiba kwani hapakuwepo na sababu yoyote ya msingi kuzuia tyukio la kikatiba kutekeleza tukio jingine la kikatiba kwa siku hiyo."Kiongozi akikwambia fanyeni hivi, fanyeni alivyoagiza baadae mjadiliane." anasema Likwati

Wito huu unaungwa mkono na Viongozi wa Dini, ambao wanasema Maadili Mema ndio nguzo ya jamii. 

"Katika Uislamu, tunafundishwa subira na kutafuta suluhu kwa njia ya amani na mashauriano. Kuchukua mali ya mtu mwingine bila haki ni dhambi kubwa." Kadhalika, pia kiongozi mmoja wa Kikristo anaongeza: "Biblia inatufundisha upendo kwa jirani, na haki inapaswa kutafutwa kwa njia ya amani. Kufanya vurugu ni kutengeneza makosa juu ya makosa." 

Aidha wataalamu wanahimiza matumizi ya Mashauriano na Upendo kama njia pekee ya kujenga taifa imara, huku tukiheshimu sheria na taratibu.