Breaking News

UMUHIMU WA MARIDHIANO YA KUJIFUNZA KUTOKA KWA WENZETU

Baada ya taharuki, hatua muhimu ni kuanzisha mchakato wa Maridhiano ya Kitaifa. Lengo ni kuwezesha jamii, kisiasa, na kidini kuketi pamoja, kujadili maumivu, kusamehe, na kuahidi kusonga mbele kwa pamoja.

Mifano ya kimataifa inaonesha faida za maridhiano ni Afrika Kusini ilitumia Tume ya Ukweli na Maridhiano (TRC) kuponya majeraha ya ubaguzi wa rangi, na Rwanda (baada ya mauaji ya kimbari) imejenga upya Taifa lake kwa misingi ya umoja na maridhiano.

Mmmoja wa wanasiasa Mkongwe anasema: "Maridhiano siyo kuficha matatizo, bali ni kuyajadili kwa uwazi na upendo, na kuamua kwa pamoja kuwa hatutaruhusu kugawanywa tena." Maridhiano yanahitaji utashi wa kisiasa na utulivu wa kimoyo. Wananchi wanataka kuona viongozi wao wakionyesha mfano wa kuweka tofauti za kando na kuungana.

Wananchi wanatoa kauli hizo wakati tayari Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za mchakato wa mazungumzo ya maridhiano ili kuwa na Taifa lenye amani na umoja na kuendelea kuwa mfano wa utulivu katika Afrika na Dunia kwa ujumla.

Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Tanzania ni salama na tulivu na ipo tayari kuendelea kupokea wageni kutoka duniani kote kwa manufaa ya nchi zote. 

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika (SADC), uliyofanyika kwa njia ya mtandao, akiwa mkoani Dodoma.

Amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuhakikisha Tanzania inapata maendeleo na amani kuendelezwa.