Breaking News

MAHAKAMA KUU ZANZIBAR KANDA YA PEMBA KUSIKILIZA KESI YA ACT WAZALENDO KUHUSU MADAI YA UKIUKWAJI WA UCHAGUZI 2025

Mahakama Kuu ya Zanzibar Kanda ya Pemba leo inatarajiwa kusikiliza kesi ya kulalamikia wasimamizi wa Uchaguzi pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, inayohusu madai ya ukiukwaji wa sheria za uchaguzi na matumizi ya nguvu za dola katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kesi hiyo imefunguliwa na waliokuwa wagombea wanane (8) wa Uwakilishi kupitia Chama cha ACT WAZALENDO, na inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo saa tatu asubuhi.

Walalamikaji hao wanatoka katika majimbo ya Konde, Micheweni, Kojani, Chakechake, Wawi, Mkoani, Chonga na Kiwani.

Kwa mujibu wa walalamikaji, wameamua kufungua kesi katika Mahakama Kuu baada ya kuhisi kuwa hawakutendewa haki katika mchakato wa uchaguzi uliopita.
“Tumeamua kwenda mahakamani kwa sababu kulikuwepo ubadhirifu na dhulma kubwa. Tunaweza kusema wazi kuwa hakukuwa na uchaguzi wa haki,” alisema mmoja wa walalamikaji.

Walalamikaji hao wanadai kuwa katika baadhi ya maeneo, visanduku vya kura vilichukuliwa bila kuhesabiwa, huku mawakala wa ACT Wazalendo wote wakiwekwa chini ya ulinzi wakati wa zoezi la kuhesabu kura, jambo ambalo, kwao, linakiuka misingi ya uchaguzi huru na wa haki.