UMOJA WA WAJASIRIAMALI DAR WAITAKA JAMII KUJIEPUSHA NA VURUGU
Dar es Salaam - Umoja wa Wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam umewataka Watanzania kujiepusha na vitendo vya vurugu vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa, ukisisitiza kuwa machafuko hayaleti tija wala suluhu ya kudumu kwa changamoto za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari, umoja huo umesema unapinga vikali wito wowote wa uchochezi unaotolewa na wanaharakati wa ndani na nje ya nchi kwa maslahi binafsi, wakidai vitendo hivyo hulitumbukiza taifa kwenye hofu, hasara za kiuchumi na kuvuruga mshikamano wa kitaifa.
Wajasiriamali hao wamesema wamefuatilia kwa karibu matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na kubaini kuwepo kwa watu waliokuwa nyuma ya pazia wakihamasisha vitendo hivyo. Kwa mujibu wao, matukio hayo yameacha funzo kubwa kwa jamii kuwa uvunjifu wa amani hauwezi kuleta maendeleo.
“Matukio ya Oktoba 29 yametosha kuwa somo. Tumeshuhudia athari zake na tumejifunza kuwa vurugu hazileti maendeleo wala suluhu ya amani,” walisema kwa pamoja.
Umoja huo umeeleza masikitiko yao makubwa na kulaani kwa nguvu zote vitendo vya uchochezi, huku ukiwasihi vijana wa Kitanzania, hususan wa kizazi cha Gen Z, kutowasikiliza watu wanaohamasisha vurugu, wakiwemo baadhi ya viongozi wa ndani, wanasiasa na wanamitandao wanaodaiwa kutumia mazingira hayo kwa maslahi binafsi au kisiasa.
Alisema waathirika wakubwa wa vurugu za Oktoba 29 walikuwa ni wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo, waliopata hasara kubwa kutokana na uharibifu wa mali na kusimama kwa shughuli za kiuchumi.
“Tutaendelea kupaza sauti kupinga uchochezi. Tutapinga wanaharakati wanaojificha nje ya nchi kuhamasisha vurugu na maandamano, tutawakemea wanamitandao wanaoeneza chuki, wanasiasa wanaochochea vurugu na hata viongozi wa dini wanaochanganya siasa na majukwaa ya kiimani,” limeeleza tamko hilo.
Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali, Mzee Omary Suleiman, mfanyabiashara wa Soko la Kinondoni, amesema vurugu hizo zilitokana na uchochezi wa makusudi na kusisitiza kuwa ni wajibu wa kila Mtanzania kuhakikisha matukio kama hayo hayajirudii.
“Tanzania ni mimi, na mimi ni nchi. Tunaomba Watanzania wote waunge mkono jitihada hizi ili Tanzania ibaki salama, yenye amani na utulivu,” alisema.
Kipitia Tamko hilo pia wameelezea ushirikiano kati ya umoja huo na Taasisi ya MICIRA, inayotoa elimu ya uraia kwa wafanyabiashara, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa haki, wajibu na umuhimu wa kulinda amani ya taifa.
Baadhi ya Wafanyabiashara waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Husein Bambe, Kiongozi wa Wajasiriamali Ubungo; Bakari Sufia wa Ilala; na Pelagia Michael, Makamu Mwenyekiti wa Wajasiriamali Kinondoni, ambao kwa pamoja walisisitiza kuwa amani ni msingi wa biashara, maendeleo na ustawi wa Taifa la Tanzania.





