NECTA YATANGAZA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2025, UFAULU WAONGEZEKA
Dar es Salaam — Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limetangaza rasmi matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne wa mwaka 2025, uliofanyika kuanzia Novemba 17, 2025.
Matokeo hayo yametangazwa leo Jumamosi, Januari 31, 2026, na Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohammed, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Profesa Mohammed, jumla ya watahiniwa 569,883 walifanya mtihani huo wakiwa wamesajiliwa katika shule 5,864 kote nchini. Aidha, watahiniwa wa kujitegemea 25,927 walifanya mtihani huo katika vituo 813.
Taarifa ya NECTA ya Novemba 16, 2025, ilibainisha kuwa idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa asilimia 7.67 ikilinganishwa na mwaka 2024. Kati ya watahiniwa wa shule 569,914 waliosajiliwa, wavulana walikuwa 266,024 sawa na asilimia 47, huku wasichana wakiwa 303,859 sawa na asilimia 53.
Mahudhurio ya watahiniwa katika mtihani huo yalikuwa asilimia 97.5, sawa na wanafunzi 555,606 waliohudhuria mtihani.
Takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu umeongezeka kwa asilimia 2.61 na kufikia asilimia 94.98, ambapo watahiniwa 526,620 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.
Aidha, idadi ya watahiniwa waliopata daraja la kwanza hadi la tatu imeongezeka na kufikia wanafunzi 255,404, sawa na asilimia 46.1 ya watahiniwa wote waliofaulu.
NECTA imeeleza kuwa matokeo hayo yanaonesha jitihada zinazoendelea za kuboresha elimu ya sekondari nchini na kuhimiza wadau wa elimu kuendelea kushirikiana katika kuinua viwango vya elimu.




