Breaking News

MAREKANI YAKATAA MSAMAHA WA JENERALI MUHOOZI WA UGANDA

Seneta wa Marekani Jim Risch, ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Mahusiano ya Kigeni, amekataa msamaha wa umma uliotolewa na Jenerali Muhoozi Kainerugaba wa Uganda, akiutaja kuwa usio na maana na usiojitosheleza huku akitoa wito wa kutaka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Uganda.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Januari 30, Risch alisema Muhoozi, mtoto wa Rais Yoweri Museveni, amevuka mstari mwekundu licha ya kufuta ujumbe wenye utata kwenye mitandao ya kijamii na kuomba msamaha kwa Marekani.

Kwa mujibu wa mwenyekiti, Marekani itatathmini upya ushirikiano wake wa kiusalama, unaojumuisha vikwazo na ushirikiano wa kijeshi na Uganda.

Seneta wa Marekani aliongeza kuwa nchi yake "haitavumilia hali ya mashaka kiwango hiki na uzembe".

Jenerali Muhoozi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Rais Museveni kuhusu oparesheni maalumu za kijeshi, alidai kuwa uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini Uganda ulihusika kumsaidia Kyagulanyi kuondoka nyumbani kwake Magere, Wilaya ya Wakiso, wakati wa operesheni ya kijeshi iliyofanyika usiku wa Januari 16, 2026.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jenerali Muhoozi alisema:

"Wananchi wenzangu wa Uganda, kutokana na hali ya sasa ambapo kiongozi wa upinzani amejiteka mwenyewe na kutoweka, na kwa mujibu wa taarifa zetu bora za kijasusi, vitendo hivi vilifanyika kwa ushirikiano na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani nchini mwetu. Kwa sababu hiyo, UPDF imesitisha ushirikiano wote na uongozi wa sasa wa Ubalozi wa Marekani jijini Kampala. Hii inajumuisha pia ushirikiano wetu nchini Somalia. Ushirikiano wa kiusalama uliokuwa wa thamani kubwa kati ya Uganda na Marekani umeathiriwa vibaya tangu mwaka 2015 na watendaji wa urasimu wasio na ubunifu katika ubalozi huo".

Baadaye, Jenerali Muhoozi alifuta ujumbe huo na kutoa radhi kwa kauli zake.