RAIS SAMIA ATOA MAELEKEZO YA UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA ELIMU
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI na wizara nyingine zinazoshughulika na elimu kuhakikisha utekelezaji kamili wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Amesema wizara husika lazima zihakikishe mkakati huu unatekelezwa kikamilifu katika ngazi zote ili kuleta matokeo yanayopimika na yenye manufaa kwa watoto na taifa.
Rais amesisitiza kuwa mkakati huu haupaswi kubaki kwenye makaratasi bali lazima ulete matokeo halisi, ikiwemo kuhakikisha watoto wa darasa la pili wanaopanda darasa la tatu wanamudu kusoma, kuandika na kuhesabu kama ilivyopangwa. Aidha, ameelekeza tathmini za maendeleo zifanyike mapema ili kubaini watoto wenye changamoto na kuwapatia msaada kwa wakati, huku akisisitiza uwajibikaji wa walimu, wakuu wa shule na maafisa elimu katika kufuatilia utekelezaji wa mkakati huu.
Rais Samia ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kushirikiana kikamilifu na serikali katika kufanikisha mpango huu. Amesema serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mkakati, kuhakikisha rasilimali na mifumo vinakwenda sambamba na matokeo yaliyokusudiwa. Vilevile, amempongeza Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda, na timu yake kwa kazi nzuri waliyoanza na kuwataka waendelee kwa bidii bila kumuangusha.




