Breaking News

UHUSIANO WA TANZANIA NA CHINA WAZIDI KUIMARIKA KUFUATIA ZIARA YA WAZIRI WANG YI

Na Mwandishi Wetu - Uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kihistoria kati ya Tanzania na China unatarajiwa kuendelea kuimarika zaidi kufuatia ujio wa kiongozi mkubwa wa China, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Wang Yi, anayefanya ziara rasmi nchini kuanzia Januari 9 hadi 10, 2026. 

Ziara hiyo inatajwa kuwa na umuhimu mkubwa katika kuendeleza ushirikiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili yenye historia ndefu ya urafiki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Wang Yi atapokelewa rasmi na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo. 

Katika ratiba ya ziara hiyo, kiongozi huyo wa China pia anatarajiwa kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo masuala ya kuimarisha zaidi ushirikiano wa pande mbili yatajadiliwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ziara ya Mhe. Wang Yi inalenga kuendeleza na kudumisha uhusiano wa kihistoria na wa kimkakati uliopo kati ya Tanzania na China, sambamba na kufuatilia utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano yaliyofikiwa katika vikao vya kimataifa, hususan Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliofanyika Beijing, China, Septemba 2024.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania na China zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu. 

Kwa takwimu za mwaka 2024, thamani ya biashara kati ya mataifa hayo mawili ilifikia takribani dola za Marekani bilioni 5.2, hatua inayoonyesha ukuaji mkubwa wa mahusiano ya kiuchumi.

Kwa upande wa uwekezaji, Kampuni za China zimeendelea kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo viwanda, kilimo, huduma, usafirishaji, mawasiliano na utalii.

Taarifa zinaonesha kuwa mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili miradi 343 ya uwekezaji kutoka China yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.1, miradi iliyochangia kuzalisha ajira zaidi ya 82,000 kwa Watanzania.

Mbali na biashara na uwekezaji, ushirikiano wa Tanzania na China umejikita pia katika sekta ya miundombinu, hususan reli ya TAZARA ambayo imeendelea kuwa alama ya urafiki na mshikamano wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili. 

Reli hiyo yenye urefu wa kilomita 1,860, ikihusisha kilomita 975 upande wa Tanzania na kilomita 885 upande wa Zambia, imekuwa kielelezo cha ushirikiano wa kweli uliolenga kuimarisha umoja na maendeleo ya kikanda.

Taarifa hiyo imebainisha kuwa ziara ya Mhe. Wang Yi ni uthibitisho mwingine wa dhamira ya mataifa hayo mawili kuendeleza urafiki uliowekwa misingi yake na waasisi wa mataifa hayo, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania na Hayati Mwenyekiti Mao Zedong wa China. 

Msingi huo umeendelea kuenziwa na kuimarishwa kizazi hadi kizazi kwa manufaa ya wananchi wa pande zote mbili.