Breaking News

NGOME YA VIJANA ACT WAZALENDO YATOA MAPENDEKEZO CHANGAMOTO ZA VIJANA NCHINI

Dar es Salaam. — Ngome ya Vijana ya ACT Wazalendo imetaka kuundwa kwa mifumo imara ya kisheria na kitaasisi ili kuimarisha uwezeshaji wa vijana kiuchumi nchini, ikionya kuwa bila kufanya hivyo, mabilioni ya fedha yanayotengwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana yataendelea kupotea bila kuleta tija iliyokusudiwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa ACT Wazalendo, Abdul Omary Nondo, amesema kuwa licha ya vijana chini ya umri wa miaka 35 kuunda takribani asilimia 70 ya idadi ya watu nchini na zaidi ya nusu ya nguvu kazi, bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira na mitaji.

Kwa mujibu wa takwimu za utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2021 na tafiti mbalimbali za kiraia, takribani vijana milioni moja huingia kwenye soko la ajira kila mwaka, lakini ni takribani vijana 200,000 pekee wanaofanikiwa kupata ajira katika sekta rasmi. Hii inaacha zaidi ya vijana 800,000 wakibaki nje ya mfumo rasmi wa uzalishaji, wengi wao wakiishia katika sekta isiyo rasmi.

Hoja kuhusu Shilingi Bilioni 200 za Vijana

Ngome ya Vijana imeeleza wasiwasi wake kuhusu Shilingi Bilioni 200 zilizotolewa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya mikopo ya vijana mapema mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, fedha hizo zilikabidhiwa na Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, kwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nnauka, kabla ya kusambazwa katika wizara mbalimbali za kisekta ikiwemo Kilimo, Mifugo, Madini, Viwanda na Biashara pamoja na Maendeleo ya Jamii.

Hata hivyo, Ngome ya Vijana imehoji utaratibu uliotumika kugawa fedha hizo nje ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund), kinyume na muongozo wa mwaka 2022 unaotaka fedha zote za uwezeshaji vijana kupita kwenye akaunti maalum ya mfuko huo.

“Mashaka makubwa yapo kuhusu uwazi, uwajibikaji na mifumo ya ufuatiliaji wa fedha hizi. Hakuna mwongozo unaoeleweka kwa vijana kuhusu namna ya kuomba, kupata na kurejesha mikopo hiyo,” imeeleza taarifa hiyo.

Changamoto za Mikopo ya Asilimia 10 Halmashauri

Mbali na fedha za Serikali Kuu, Ngome ya Vijana imegusia changamoto za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu (4+4+2), chini ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.

Kwa mujibu wa taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), mfumo wa utoaji na urejeshaji wa mikopo hiyo umekuwa ukikumbwa na urasimu, vikundi hewa, makusanyo hafifu na ukosefu wa uwajibikaji wa kutosha.

Ngome ya Vijana imesema hata baada ya majaribio ya kushirikisha taasisi za kifedha katika baadhi ya halmashauri, bado mfumo haujawa thabiti kiasi cha kuondoa dosari zilizopo.

Mapendekezo: Kuundwa kwa Wakala Maalum

Katika mapendekezo yake, Ngome ya Vijana imetaka kuundwa kwa chombo maalum cha kisheria kitakachoitwa Wakala wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi Tanzania (Tanzania Youth Economic Empowerment Agency – TYEA) chini ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana.

Kwa mujibu wa pendekezo hilo, wakala huo utakuwa na jukumu la kuratibu utoaji na urejeshaji wa mikopo, kufuatilia miradi ya vijana, kutoa ushauri wa kitaalamu, kuhamasisha fursa na kuhakikisha mifumo ya uwajibikaji inaimarishwa kuanzia ngazi ya taifa hadi mikoa na wilaya.

Ngome ya Vijana imeeleza kuwa mfano wa chombo kama hicho upo katika Afrika Kusini kupitia taasisi ya National Youth Development Agency inayoratibu masuala ya vijana kiuchumi chini ya wizara husika.
Aidha, imetaka kutungwa kwa Sheria ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (Youth Development Fund Act) badala ya kuendelea kutumia muongozo wa mwaka 2022 ambao hauna nguvu ya kisheria.

Wito wa Uwazi na Uwajibikaji

Ngome ya Vijana imesisitiza kuwa badala ya viongozi kugawa mikopo moja kwa moja katika ziara za mikoani, ni muhimu kuweka mifumo ya kudumu ya sera, sheria, uratibu na tathmini itakayohakikisha fedha za vijana zinawafikia walengwa kwa haki na uwazi.

“Tunahitaji mifumo, si matukio. Uwezeshaji wa vijana hauwezi kuwa wa majaribio au wa hiari ya mtu binafsi. Lazima uwe wa kisheria, wa kitaasisi na unaoweza kufuatiliwa,”alisisitiza Bw. Nondo