Breaking News

TANESCO NA REA; WANANCHI WANAOLIPIA UMEME WAUNGANISHWE KWA WAKATI - MHE. SALOME

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha kuwa wateja wote wanaolipia huduma ya umeme wanaunganishwa kwa wakati ili kuwawezesha kuutumia kwa shughuli za kijamii na kiuchumi.

Ametoa agizo hilo tarehe 23 Februari 2026 mara baada ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Bugofuma, kilichopo Kijiji cha Ngeleka wilayani Misungwi mkoani Mwanza, ambacho kimepata umeme kupitia mradi unaotekelezwa na TANESCO kwa gharama ya shilingi milioni 174, huku wateja wa awali 171 wakitarajiwa kunufaika.

“Sisi Wizara ya Nishati tumeshawaelekeza REA na TANESCO kuhakikisha kuwa katika miradi ya umeme vitongojini inayoendelea mtu akilipia leo, zisipite siku tatu hadi nne awe amewekewa umeme. Na hapa Bugofuma tumeona TANESCO wametekeleza agizo hili kwani kati ya wananchi wa awali 35 waliolipia huduma jana, tayari wananchi 22 wameunganishiwa umeme”. Amesema Mhe. Salome