Breaking News

TNCC NA MABORESHO YA BIASHARA

Wakati Serikali ikishughulikia uwekezaji mkubwa, Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) imeanza kikao kazi cha ndani jijini Dodoma kuboresha utendaji wake ili kuhakikisha wafanyabiashara wadogo na wa kati wanapata uwakilishi imara na utatuzi wa kero zao.

Akifungua kikao hicho, Rais wa TNCC, Vicent Minja, alisema chemba hiyo inajipanga kuwa daraja imara kati ya wafanyabiashara na mamlaka za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZA/TISEZA) ili kupunguza migongano ya kodi na sera.

“Kila tunachokiboresha ndani ya TNCC kina lengo la kumrahisishia mfanyabiashara mazingira ya kufanya kazi. Tunataka kuhakikisha sera na mifumo ya kodi inaeleweka vizuri na inatumika kama chachu ya ukuaji badala ya kuwa kikwazo,” alisema Minja.

Naye Meneja Maendeleo ya Biashara wa TNCC, Mercy Philipo, aliongeza kuwa taasisi hiyo inapitia mifumo yake ya kidijiti na huduma ili kuhakikisha inakuwa karibu na wafanyabiashara nchi nzima, ikitoa taarifa sahihi za fursa za uwekezaji kwa wakati.

UBUNIFU DHIDI YA KEJERI 

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wameeleza kuwa hatua hizi za Serikali na sekta binafsi ni jibu tosha kwa vijana wanaotafuta fursa za kiuchumi. Badala ya kupoteza muda katika kejeli za mitandaoni, ujenzi wa migodi kama Nyanzaga na maboresho ya mifumo ya biashara kupitia TNCC yanatengeneza njia rasmi ya ajira na ujasiriamali kwa wenye ujuzi na nia ya kufanya kazi.

Ushirikiano huu wa kimkakati kati ya Wizara ya Fedha, wawekezaji wa nje, na Chemba ya Biashara unadhihirisha kuwa mazingira wezeshi ya Tanzania sasa yamefikia kiwango cha kuvutia mitaji mikubwa na kutoa ajira za uhakika kwa Watanzania.