MJUMBE MAALUM WA UN AIPONGEZA TANZANIA KWA JUHUDI ZA KUIMARISHA AMANI NA TAASISI ZA KIDEMOKRASIA
Dar es Salaam — Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa katika Umoja wa Afrika (UNOAU), Bw. Parfait Onanga-Anyanga, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua ilizochukua kurejesha amani na utulivu kufuatia vurugu na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea katika baadhi ya maeneo nchini tarehe 29 Oktoba 2025.
Bw. Onanga-Anyanga, ambaye pia ni mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alitoa pongezi hizo wakati wa mazungumzo yake na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, jijini Dar es Salaam. Mazungumzo hayo ni sehemu ya mwanzo wa mashauriano yake na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wa kitaifa.
Mjumbe huyo yupo nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kufanya mashauriano na Serikali na wadau wengine kuhusu hali ya kisiasa nchini, pamoja na kujadili namna Umoja wa Mataifa unavyoweza kuunga mkono juhudi za kuimarisha taasisi za kidemokrasia, kusimamia mageuzi na kuendeleza umoja na mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano jumuishi.
Katika mazungumzo hayo, Bw. Onanga-Anyanga alimpongeza pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake wa utulivu na makini wakati wa kipindi kigumu kilichofuata matukio ya vurugu baada ya uchaguzi.
Aidha, alikaribisha uamuzi wa Serikali wa kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman. Alisema muundo wa tume hiyo unaojumuisha wataalamu kutoka kada mbalimbali umeongeza ubora, uhuru na kuifanya kuwa mfano wa viwango vya kimataifa.
Bw. Onanga-Anyanga pia aliipongeza Serikali kwa juhudi zake za kurejesha imani ya wananchi na kudumisha utulivu baada ya matukio hayo, pamoja na namna changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha uchaguzi zilivyoshughulikiwa kwa hekima na utulivu.
Katika hatua nyingine, alikaribisha mpango mpana wa kitaifa uliotangazwa Januari 2026 chini ya kaulimbiu “Repair, Rebuild, Renew”, akieleza kuwa mpango huo unaweka msingi muhimu wa kuimarisha utawala wa kidemokrasia, kusimamia mageuzi ya taasisi na kuendeleza maridhiano ya kitaifa.
Vilevile alimpongeza Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo, kwa juhudi zake za kuielezea jumuiya ya kimataifa hatua zinazochukuliwa na Tanzania kushughulikia matukio hayo na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika ratiba ya ziara yake, Bw. Onanga-Anyanga anatarajiwa kukutana na viongozi wa vyama vya siasa ikiwemo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ACT Wazalendo, Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya utawala bora, demokrasia na mshikamano wa kitaifa.
Pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge, Jaji Mkuu pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wawakilishi wa mihimili mitatu ya dola.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje Mahmoud Thabit Kombo ameishukuru Umoja wa Mataifa kwa ushirikiano wake na kusisitiza kuwa Tanzania inauthamini sana ushirikiano huo. Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na UN na haitasita kuomba msaada wake inapohitajika katika kuimarisha taasisi za taifa na kulinda amani, utulivu na mshikamano wa wananchi.











