Breaking News

RAIS SAMIA: NGORONGORO NI ALMASI YA TANZANIA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amewaelekeza Katibu Mkuu Kiongozi pamoja na Waziri Mkuu kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Kutathimini Uhamaji wa Hiari katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na kuhakikisha yale yote yaliyopendekezwa yanafanyiwa kazi na rasilimali zinazotakiwa kwenye utekelezaji wa mapendekezo hayo zinapatikana.

Kauli hiyo ameitoa leo Machi 12, 2026, Ikulu Chamwino jijini Dodoma, wakati akizungumza kwenye hafla ya kupokea taarifa za tume za masuala ya ardhi.

Rais Samia ameeleza kuwa anatambua kuwa mchakato wa utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na tume hiyo unaweza kuibua maoni tofauti katika jamii lakini pia taasisi nyingine na watu ambao wana maslahi na Ngorongoro.

Hivyo, Rais Samia amewaomba Watanzania wote kulipa kipaumbele suala la uendelevu wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na maeneo mengine ya hifadhi nchini.

"Ngorongoro ni almasi yetu Tanzania, ni mali yetu Tanzania, lakini pia ni urithi wa dunia. Wale wote wanaoleta maneno kwa faida zao, kwa wanayoyaona wao, sisi Ngorongoro Mungu ameishusha kwetu Tanzania. Hatuna budi kuienzi tunu hii ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia," amesema Rais Samia.

Source Tbc Digital