Breaking News

RAIS DKT. MWINYI: FUTARI YA KITAIFA ZANZIBAR NI HISTORIA YA UMOJA NA MSHIKAMANO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa Zanzibar imeandika historia ya kipekee kwa kuandaa Tukio Kubwa la Futari ya Kitaifa kwa mara ya kwanza, lililowakusanya maelfu ya Waumini wa Dini ya Kiislamu katika mkusanyiko wa pamoja.

Alhaj Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 07 Machi 2026 alipotoa salamu zake kwa maelfu ya Waumini wa Dini ya Kiislamu waliohudhuria Futari hiyo ya Kitaifa iliyofanyika katika Uwanja wa New Amaan Complex, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema tukio hilo ni jambo jema lenye thawabu kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, sambamba na kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi kwa ujumla katika kuimarisha mshikamano, upendo na umoja.

Aidha, Alhaj Dkt. Mwinyi amezishukuru taasisi za Serikali zilizoshirikiana kufanikisha Futari hiyo ya Kitaifa, ambazo ni Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), kwa juhudi zao za kuandaa tukio hilo kubwa lililowakutanisha Waumini wengi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Katika nasaha zake, Rais Dkt. Mwinyi amewataka Waumini kuendelea kuzidisha ibada, dua na matendo mema katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, huku wakiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kuijalia nchi amani, utulivu na mshikamano miongoni mwa wananchi wake.

Kwa upande wake, Naibu Mufti wa Zanzibar, Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, amesema Futari hiyo ya Kitaifa ni tukio muhimu linaloongeza mapenzi na upendo miongoni mwa Waumini, huku likichangia kuondoa chuki na kuimarisha mshikamano kati ya makundi mbalimbali ya Waumini wa Dini ya Kiislamu.