WANYAMAPORI WAMEUA WATU 77, KUJERUHIi 274 NGORONGORO
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro, Gerald Mbita, amesema wastani wa watu saba wamekuwa wakiuawa na wanyamapori kila mwaka kuanzia mwaka 2015 hadi 2025 katika eneo la Ngorongoro Conservation Area, na kufanya idadi ya watu waliouawa kufikia 77.
Dkt. Mbita amesema pia watu 274 wamejeruhiwa huku mifugo 1,450 ikiuawa na wanyamapori katika eneo hilo la hifadhi.
Ametoa takwimu hizo katika hafla ya kupokea taarifa za pamoja za Tume ya Rais ya Kutathmini Mgogoro wa Ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro na Tume ya Rais ya Kutathmini Zoezi la Uhamaji wa Hiari wa Wakazi wa eneo hilo, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Machi 12, 2026.
Aidha, Dkt. Mbita amesema tafiti zinaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2000 baadhi ya wanyamapori kama choroa, nyamela na swala twiga wametoweka ndani ya eneo la Ngorongoro Conservation Area, huku nyumbu wakazi wakitajwa kupungua.
Kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo kunatajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea kutoweka kwa baadhi ya wanyamapori.
Source Tbc Digital




