SHEIKH JALALA AHIMIZA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO BAADA YA EID AL-FITR
Sheikh mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC) Maullana sheikh Hemed Jalala akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya Swala ya Eid Al-Fitr iliyofanyika katika Masjid Ghadiir Kigogo Post jijini Dar es salaam.
Dar es Salaam – Wananchi wametakiwa kuendelea kuenzi na kuhubiri amani, mshikamano na umoja wa taifa baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza baada ya Swala ya Eid Al-Fitr, Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala, amesema kuwa kipindi cha Ramadhani kilikuwa na amani, mshikamano na umoja katika sehemu zote za nyumba za ibada na jamii kwa ujumla. Alisisitiza umuhimu wa kuendeleza hali hiyo baada ya sikukuu.
“Katika kipindi chote cha mfungo wa mwezi wa Ramadhani, amani, umoja na mshikamano vilikuwa vinatawala sehemu zote za nyumba za ibada na sehemu zote hapa nchini. Basi ni jukumu letu kuendelea kuenzi na kuhubiri amani na umoja wetu ili taifa liendelee kuwa na amani,” alisema Sheikh Jalala.
Sheikh Jalala pia aliongeza kuwa nchi yetu imebarikiwa kwa uwepo wa amani, mshikamano na umoja, na kwamba kila raia ana wajibu wa kulinda tunu hii muhimu ili idumu kwa vizazi vijavyo.
Alisema ni muhimu kuendeleza maadili ya amani na mshikamano katika maisha ya kila siku, si tu wakati wa sikukuu za kidini, bali katika kipindi chote cha mwaka.








