AMANI NI FURSA: VIJANA WAIMIZWA KULINDA AMANI NA KUCHANGAMKIA FURSA
Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, ametoa wito maalumu kwa vijana kujikita katika kulinda amani huku wakichangamkia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali, hususan tiba asili na uhifadhi wa mazingira.
Akizungumza kupitia ujumbe wake maalumu kwa vijana, Mwalongo amesema kuwa dunia ya sasa imejaa fursa nyingi za maendeleo, lakini upatikanaji wake unategemea uwepo wa amani, umoja na mshikamano katika jamii.
Amesisitiza umuhimu wa vijana kuwa mabalozi wazuri wa maadili kwa kuzingatia sheria na usalama, hasa katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Ameonya kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mitandao yanaweza kuhatarisha usalama na kusababisha migogoro ya kijamii pamoja na kuathiri taswira ya jamii.
Aidha, akizungumzia mchango wa amani katika maendeleo, Mwalongo amesema kuwa vijana wanapaswa kutumia maarifa, ubunifu na uthubutu wao kuzitumia kikamilifu fursa zilizopo badala ya kusubiri ajira rasmi.
“Anza kidogo, lakini anza leo. Maendeleo ya kweli huanza na hatua ndogo ya uthubutu,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, ametoa wito kwa wabunge vijana duniani kutumia nafasi zao kushinikiza ajenda ya tiba asili katika sera na sheria, ili kuitambua rasmi kama sekta yenye mchango mkubwa katika uchumi, elimu na utafiti wa kisayansi.
Amehitimisha kwa kueleza kuwa sekta ya tiba asili na uhifadhi wa mazingira ni fursa muhimu kwa vijana, ambazo zikitumiwa kwa weledi zinaweza kuchangia kujenga uchumi imara, kuboresha afya za jamii na kuhifadhi urithi kwa vizazi vijavyo.




