Breaking News

MAMA LISHE : AMANI NA UTULIVU NI NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA

Wazazi na walezi wametakiwa kutambua kuwa amani na utulivu ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa, huku chimbuko la amani likianzia katika ngazi ya familia.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Bi. Yusra Ismail, ambaye anajishughulisha na shughuli za mama lishe, amesema kuwa jukumu la kujenga misingi ya amani linaanzia nyumbani. Alieleza kuwa wazazi na walezi wanapaswa kuwafundisha watoto wao maadili ya upendo, utulivu na mshikamano tangu wakiwa wadogo.

“Bila kuwepo kwa amani ndani ya familia, ni vigumu kufikia maendeleo ya kweli au kutekeleza mipango yoyote ya kimaendeleo katika jamii,” alisema Bi. Yusra.

Aliongeza kuwa amani huunganisha familia na jamii kwa ujumla, na ndiyo inayochochea maendeleo endelevu. Aidha, aliwahimiza wananchi kuilinda amani iliyopo kwa nguvu zote ili kuhakikisha inaendelea kudumu.

“Ndugu zangu, tuilinde amani yetu. Amani huleta watu pamoja na huchochea maendeleo ya taifa,” alisisitiza.

Bi. Yusra pia alibainisha kuwa katika siku za hivi karibuni, viongozi wa nchi wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa amani, umoja na upendo, akieleza kuwa hayo ndiyo maadili yanayoongoza safari ya maendeleo ya taifa.

Alifafanua kuwa taifa lenye amani hupata heshima kubwa kimataifa na hujenga mazingira mazuri ya uwekezaji na ustawi wa wananchi wake.