Breaking News

MANGU AWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA AMANI NA MSHIKAMANO

Mkuu wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu, ametoa wito kwa Watanzania kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na badala yake kuendeleza mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa amani ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mangu alisema kuwa ishara zozote za kuchochea vurugu au kuvuruga utulivu wa nchi zinapaswa kukemewa mapema, akionya kuwa gharama za kupoteza amani ni kubwa na huathiri sekta zote za uchumi na ustawi wa jamii.

“Tuna wajibu wa kulinda amani yetu. Historia inaonyesha kuwa pale amani inapovunjika, athari zake huwa pana, zikigusa uchumi, uwekezaji na maisha ya watu kwa ujumla,” alisema.

Mangu alieleza kuwa Tanzania imejijengea sifa ya kuwa nchi yenye utulivu kwa muda mrefu, hali ambayo imeiwezesha kuvutia uwekezaji na kukuza shughuli za kijamii na kiuchumi. Aliongeza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kulindwa na kuendelezwa kupitia uwajibikaji wa wananchi na taasisi zote.