TMA YATOA TAADHARI YA MVUA KUBWA KATIKA BAADHI YA MIKOA YA UKANDA WA PWANI, IKIHUSISHA DAR
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya siku tatu kuhusu uwezekano wa kunyesha kwa mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko katika baadhi ya mikoa ya ukanda wa pwani, ikiwemo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Aprili 7, 2026, mvua hizo zinatarajiwa kuanza siku ya Jumatano hadi Ijumaa. Maeneo yatakayoathirika ni pamoja na mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Dar es Salaam, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA imeeleza kuwa kiwango cha uwezekano wa mvua hizo na athari zake kimeainishwa kuwa cha kati, lakini imeonya kuwa bado kuna hatari ya kutokea mafuriko katika baadhi ya maeneo. Hali hiyo inaweza kuathiri shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Kuanzia kesho hadi Ijumaa mvua zinatarajiwa kunyesha katika maeneo tajwa, huku uwezekano wa athari zake ukiwa katika kiwango cha kati,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha, wananchi wanaoishi katika maeneo ya pwani na visiwani wametakiwa kuchukua tahadhari zaidi kutokana na uwezekano wa kuongezeka kwa kiwango cha mvua.
TMA imehimiza umma kuendelea kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua hatua stahiki za kujikinga dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.
Mamlaka hiyo imeongeza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa na kutoa taarifa zaidi kadri itakavyohitajika.





