RC MTANDA APONGEZA TASAC KWA KUHAMASISHA UJENZI WA MELI NCHINI
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amepongeza juhudi za Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) za kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa meli nchini ili kukuza uchumi wa maji na kuongeza ajira kwa vijana.
Mhe. Mtanda ametoa pongezi hizo leo Mei 7, 2026 ofisini kwake alipokutana na kufanya mazungumzo na Wakili Leticia Mutaki ambaye ni Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri wa TASAC.
Amesema Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa majini kupitia miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Bandari ya Mwanza Kusini, kituo cha uangalizi na uokozi ndani ya Ziwa Victoria pamoja na kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, hatua ambazo zimeongeza fursa za uwekezaji katika sekta hiyo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema Mwanza ni eneo sahihi kwa utekelezaji wa mpango huo kwa kuwa asilimia 53 ya Mkoa huo imezungukwa na maji ya Ziwa Victoria huku maeneo ya visiwani kama Ukerewe na Buchosa yakihitaji usafiri wa uhakika na wa kutosha.
Aidha amesema mpango huo utasaidia kuongeza mwingiliano wa kiuchumi na kijamii ndani na nje ya nchi, akitolea mfano wageni kutoka nchi za Afrika Mashariki waliowahi kutembelea kituo cha Songoro Marine kilichopo Wilaya ya Ilemela na kuvutiwa na uwezo wa ujenzi wa meli, vivuko na boti unaofanyika katika eneo hilo.
Kadhalika, amesema Serikali ya Mkoa itaendelea kushirikiana na TASAC kutoa elimu na hamasa kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi wa meli kwani bado watu wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu fursa hiyo.
Kwa upande wake, Wakili Leticia Mutaki amesema TASAC imeamua kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika ujenzi wa meli ili Watanzania waweze kunufaika na fursa za uchumi wa maji badala ya kutegemea ununuzi wa meli kutoka nje ya nchi.
Amesema watu wengi wanapopata uwezo wa kifedha hujielekeza zaidi katika uwekezaji wa mabasi, huku wakisahau kuwa hata sekta ya ujenzi wa meli ina fursa kubwa za kiuchumi na ajira.
Ameongeza kuwa Tanzania ina rasilimali kubwa ya maji kupitia bahari na maziwa, hivyo sekta binafsi inapaswa kutumia fursa hiyo kuwekeza katika ujenzi wa meli na vyombo vya usafiri wa majini.








