RIPOTI YA JAJI CHANDE IMEELEZA MAHITAJI YA WANANCHI - CHAUMMA
Dar es salaam - Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu amesema Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imetekeleza wajibu wake kwa kuainisha changamoto halisi zinazowakabili Watanzania.
Amesema Kamati Kuu ya chama hicho imeridhishwa na hoja na sababu zilizotolewa na Tume hiyo iliyoongozwa na Mohamed Othman Chande kuhusu chanzo cha ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi.
“Jaji Chande amesema kuhusu Katiba mpya, amesema kuhusu Tume huru ya uchaguzi, amezungumzia suala la uchumi wa vijana na hali ya ajira, amezungumza kuhusu suala la utekaji na watu kupotea, pamoja na uwajibikaji hafifu wa viongozi katika kuwatumikia wananchi. Sisi hatuna mashaka na mambo haya, na hakuna anayeweza kukataa kuwa yaliyozungumzwa ni kero za Watanzania,” amesema Mwalimu.
Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 7, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya Kamati Kuu ya CHAUMMA kufuatia ripoti ya Tume ya Uchunguzi wa matukio ya Oktoba 29, 2025.
Amesema badala ya kupinga ripoti hiyo, chama chake kimeamua kuelekeza nguvu katika kushinikiza Serikali kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa na Tume hiyo.
“Kama hizo ndio kero zetu, tunazipinga ili iweje? Sisi tumeukataa huo mtego wa kupinga kila kitu. Badala yake, tunataka Serikali ifanyie kazi yale yaliyozungumzwa na Jaji Chande. Katiba mpya tumeidai kwa zaidi ya miaka 30, na Tume mbalimbali zimekuwa zikizungumzia mambo haya haya,” amesema.
Aidha, Mwalimu amesema upinzani unapaswa kujitathmini kuhusu namna ya kushughulikia masuala ya kitaifa, akionya dhidi ya tabia ya kupinga kila jambo bila kuangalia maslahi mapana ya wananchi.
“Nadhani wakati mwingine tunapaswa kujiuliza huwa tunakosea wapi sisi kama wapinzani. Moja ya sababu inaweza kuwa ni kutanguliza dhana kwamba kazi ya upinzani ni kupinga kila kitu. Hata wanaoipinga ripoti hii ya Jaji Chande, ipo siku wataitumia kama rejea ya masuala mbalimbali,” amesema




