SHEIKH JALALA ATOA WITO WA KULINDA AMANI, UMOJA NA MSHIKAMANO WA TAIFA
Dar es salaam - Waumini wa Kiislamu wa dhehebu la Shia Ithna'ashariyyah wameungana na Waislamu wengine duniani kuadhimisha Sikukuu ya Eid el-Hajj kwa kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kuuenzi umoja wa kitaifa, mshikamano na amani ili kulinda utulivu wa nchi.
Akizungumza mbele ya waumini wakati wa salamu za Eid, Sheikh Hemed Jalala amesema jambo kubwa ambalo Watanzania hawapaswi kulijutia ni kuvunjika kwa umoja wao wa kitaifa, akisisitiza kuwa maandiko matakatifu yameweka mkazo mkubwa juu ya mshikamano na kuishi kwa upendo.
Amesema Qur’an pamoja na vitabu vingine vya dini vinaelekeza umuhimu wa kuenzi amani huku kila mtu akidai haki zake kwa njia inayolinda utulivu wa taifa.
“Watanzania tumepewa neema kubwa ya kuishi kwa upendo bila kujali tofauti za dini. Katika mitaa yetu wanaishi Waislamu, Wakristo na watu wa imani tofauti kwa mshikamano mkubwa, jambo ambalo si la kawaida katika mataifa mengi,” amesema Sheikh Jalala.
Ameongeza kuwa tabia hiyo imejengeka hata ndani ya familia nyingi za Kitanzania ambapo watu wa dini tofauti huishi pamoja kwa amani na kuheshimiana.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kulinda maadili ya taifa akieleza kuwa kuvunjika kwa maadili na mila nzuri ni miongoni mwa sababu zinazoweza kudhoofisha maendeleo ya jamii.
Katika hotuba yake, Sheikh Jalala pia amepinga vikali madai yanayotolewa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii kwamba Tanzania kuna ukandamizaji wa kidini, akisema nchi imeendelea kuwa mfano wa uhuru wa kuabudu na usawa kwa waumini wa dini zote.
“Umoja na mshikamano wa Waislamu na Wakristo nchini ni ushahidi kuwa Tanzania hakuna ubaguzi wala ukandamizaji wa kidini,” amesema.
Pia amemuombea dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ili aendelee kuiongoza nchi kwa amani, mshikamano na utulivu. Aidha, amewaombea viongozi wengine wa serikali pamoja na wananchi kwa ujumla waendelee kushirikiana katika kudumisha amani ya taifa.









