TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA KIPUPWE JUNI – AGOSTI 2026, YATADHALISHA JUU YA UWEPO WA BARIDI KALI NA MVUA ZA NJE YA MSIMU
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa msimu wa Kipupwe wa Juni hadi Agosti mwaka 2026 unatarajiwa kuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi nchini, huku mwezi Julai ukitajwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi katika baadhi ya maeneo.
Akitoa taarifa ya mwenendo wa hali ya hewa kwa kipindi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kusini pamoja na Nyanda za Juu Kusini-Magharibi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi.
Amesema maeneo ya ukanda wa pwani ya kaskazini na kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku baadhi ya maeneo yenye miinuko yakishuhudia hali ya hewa kushuka hadi chini ya nyuzi joto 10 za sentigredi.
Kwa mujibu wa Dkt. Chang’a, msimu huo pia utatawaliwa na upepo kutoka Kusini Mashariki wenye nguvu iliyopungua kidogo, ingawa kutakuwepo vipindi vya upepo mkali zaidi katika miezi ya Juni na Julai, hususan katika maeneo ya pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.
Aidha, TMA imeeleza kuwa licha ya msimu wa Kipupwe kwa kawaida kuwa wa ukavu, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za nje ya msimu. Maeneo hayo ni pamoja na Kanda ya Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA imeonya kuwa hali ya baridi pamoja na vumbi inaweza kuongeza magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji kama mafua na homa ya mapafu, sambamba na magonjwa ya macho na yale yanayoathiri mifugo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imezitaka jamii, wakulima, wafugaji pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa pamoja na tahadhari zinazotolewa mara kwa mara ili kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli zao za kila siku.








