USALAMA WA TANZANIA NI JUKUMU LA KILA MWANANCHI
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 imelenga kuendelea kuijenga Tanzania kuwa nchi salama na yenye utulivu kwa wananchi wote.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma, Ayoub amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama wa taifa kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, sambamba na kuboresha mifumo ya kiusalama nchini.
Amesema licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali, wananchi nao wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda amani na usalama wa nchi, hususan vijana ambao wana nafasi kubwa katika kuhakikisha utulivu wa taifa unaendelea kudumu.
“Usalama wa Tanzania ni jukumu la kila mwananchi,” amesema Ayoub akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya dola katika kuzuia vitendo vya uhalifu na kulinda amani ya nchi.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuongeza uwezo wa vyombo vya dola kwa kuvipatia vifaa, teknolojia na mazingira bora ya utendaji kazi ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na usalama.
Kauli hiyo imekuja wakati Serikali ikiendelea kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao, huku ikihimiza mshikamano wa kitaifa na ushiriki wa wananchi katika masuala ya usalama wa nchi.




