VIJANA EPUKENI KAULI ZINAZOWEZA KUCHOCHEA MIGAWANYIKO - KILIBA
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu nchini (TAHLISO), Geofrey Kiliba, amesema jumuiya hiyo haiungi mkono migogoro au changamoto zinazoweza kuvuruga amani nchini, bali inaendelea kuhamasisha vijana kutumia busara, hekima na mshikamano katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili.
Kiliba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi wa serikali za wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, ambapo alisisitiza umuhimu wa vijana kuwa sehemu ya kujenga umoja na maendeleo ya taifa kupitia elimu na majadiliano yenye tija.
Amesema vijana wanapaswa kutumia majukwaa ya elimu ya juu kama fursa ya kutoa mawazo chanya na suluhu zitakazosaidia kuimarisha mshikamano wa kitaifa badala ya kuchochea migawanyiko katika jamii.
Aidha, Kiliba amekemea vitendo na kauli zinazolenga kuwagawa Watanzania, akieleza kuwa vyuo vikuu vina nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo ya kijamii na kitaifa kupitia njia za amani, mazungumzo na ushirikiano miongoni mwa wananchi.




