ALIYEKIMBIA HUKUMU YA MIAKA 20 AKAMATWA MAFICHONI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Arusha imemkamata mshtakiwa Amani Mlaya, aliyekuwa Mratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Halmashauri ya Jiji la Arusha, baada ya kutoroka mahakamani kinyume na masharti ya dhamana yake katika shauri la jinai namba 000011512 la mwaka 2024.
Akizungumza na TBC Digital, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Mangaka, Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, ambapo alikuwa amejificha baada ya kutoroka wakati wa hatua za mwisho za shauri hilo.
Amesema awali mahakama ilimkuta na hatia katika makosa manne na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo alikwepa kutekeleza hukumu hiyo kwa kutoroka siku ya kusomewa hukumu.
Ngailo ameongeza kuwa mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa huyo na kuelekeza kuwa aanze kutumikia adhabu hiyo mara baada ya kupatikana.
Mshtakiwa Amani Mlaya alikuwa akikabiliwa na jumla ya makosa sita, yakiwemo manne ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri, kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329, marejeo ya mwaka 2022, pamoja na makosa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa, Sura ya 200, marejeo ya mwaka 2022.
Source Tbc digital




