Breaking News

CHALAMILA AAGIZA KUKAMATWA MADEREVA WANAOPAKI MALORI HOVYO HIFADHI ZA BARABARA

Na Mwandishi Wetu - Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Temeke na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke kuunda kikosi kazi maalumu cha kuwakamata madereva wa malori wanaoegesha katika maeneo yasiyorasmi, hususan hifadhi za barabara.

Chalamila ametoa agizo hilo baada ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Temeke, ikiwemo Barabara ya Mandela na Kata ya Sandali, ambako alishuhudia malori mengi yakiwa yameegeshwa kwenye hifadhi za barabara na mengine yakiziba njia.

Amesema hatua hiyo inaanza kuchukuliwa rasmi dhidi ya madereva wanaokiuka maagizo yaliyotolewa awali, akisisitiza kuwa watakaokutwa wameegesha malori katika maeneo yasiyoruhusiwa wanapaswa kukamatwa na kuhojiwa kwa hatua zaidi.
Aidha, Chalamila amewataka wamiliki wa bandari kavu kuhakikisha wanaandaa maeneo maalumu ya maegesho ya malori ndani ya vituo vyao ili kuondoa tabia ya malori kuegeshwa kwenye hifadhi za barabara na kusababisha msongamano.

Ameagiza Mkuu wa Wilaya ya Temeke kuwaita wamiliki wa bandari kavu katika kikao kitakachoongozwa na Mkuu wa Mkoa kesho, Jumatano, Agosti 19, 2026, kwa ajili ya kuwapatia maelekezo zaidi kuhusu matumizi ya maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Chalamila amesisitiza mabasi yote ya mikoani na yanayokwenda nchi jirani kurejea kupaki katika Kituo cha Mabasi cha Magufuli badala ya kutumia eneo la Shekilango na maeneo mengine yasiyorasmi.
Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Dar es Salaam wa kupunguza msongamano wa magari na kuhakikisha barabara zinatumika kwa ufanisi.

Katika ziara hiyo, Chalamila pia alikagua daraja linalounganisha Kata ya Toangoma na Kata ya Kibondemaji, hususan maeneo ya Mtaa wa Golani B na Kichangani, ambapo alibaini kuwa daraja hilo lilijengwa miaka michache iliyopita na wananchi kwa nguvu zao wenyewe, lakini halikidhi viwango vinavyohitajika.

Kutokana na hali hiyo, ameiagiza TARURA kufanya tathmini ya eneo hilo mapema na kuandaa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu litakalosaidia kuondoa kero hiyo ya muda mrefu kwa wananchi.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Sandali pamoja na madereva wa malori walieleza changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maegesho rasmi ya malori, uharibifu wa mazingira unaodaiwa kusababishwa na salfa inayotoka katika bandari kavu ya eneo hilo, pamoja na ukosefu wa barabara za ndani.

Akizungumza baada ya kusikiliza changamoto hizo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jomari Mrisho Satura, amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa kilio cha wananchi pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi.