Breaking News

CDF CUP 2026 KUANZA JULAI 6, YALENGA KUIBUA VIPAJI NA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATI YA JESHI NA JAMII

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Michuano ya CDF Cup 2026, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi, amesema michuano hiyo inatarajiwa kuanza rasmi Julai 6, 2026, ikiwa na lengo la kuonesha namna Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linavyoendeleza na kuibua vipaji mbalimbali vya michezo.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya michuano hiyo, Brigedia Jenerali Saidi amesema JWTZ imejipanga kuendelea kuimarisha timu zake za michezo ili ziweze kutoa wawakilishi bora katika mashindano ya ndani na nje ya nchi.

Amesema katika michuano ya mwaka huu, jeshi limefanya maboresho mbalimbali ikiwemo kuanzisha zawadi za mikanda kwa washindi wa baadhi ya michezo pamoja na kuingiza mchezo wa Pool Table ili kuongeza wigo wa ushiriki kwa wanamichezo wengi zaidi.

Brigedia Jenerali Saidi amebainisha kuwa michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu, Pool Table, mchezo wa mishale na michezo mingine ya mikono.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Benki ya CRDB, Bi. Farida Mbwana, ameipongeza kamati ya maandalizi ya michuano hiyo kwa jitihada zake za kuendeleza michezo nchini. Amesema michezo ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii yenye mshikamano, umoja na maendeleo.

Naye mwanariadha mashuhuri wa JWTZ, Alphonce Simbu, akizungumza kwa niaba ya wanamichezo wenzake, amempongeza Mkuu wa Majeshi kwa kufanikisha uwepo wa michuano hiyo. Amesema mashindano hayo yanatoa fursa muhimu kwa wanamichezo kujiandaa kwa mashindano ya kimataifa na kuongeza kiwango cha ushindani.

Michuano ya CDF Cup 2026 inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mshikamano, uzalendo na ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama. Kupitia mashindano hayo, wananchi watapata fursa ya kushiriki na kushuhudia vipaji mbalimbali vya michezo huku wakijenga ukaribu zaidi na jeshi lao.

Mbali na kutoa burudani, CDF Cup imeendelea kutambulika kama chombo cha kukuza nidhamu, afya njema na ari ya kufanya kazi kwa pamoja. Mashindano hayo yanatarajiwa kuwakutanisha washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na hivyo kuimarisha umoja wa kitaifa kupitia michezo.

Wadau wa michezo wanatarajia CDF Cup 2026 kuacha alama kubwa kwa kuibua vipaji vipya na kuimarisha mahusiano kati ya jeshi na jamii. Ujio wa michuano hiyo unaonekana kuendeleza dhana kwamba michezo ni daraja muhimu la kuwaunganisha Watanzania kwa manufaa ya taifa.