Breaking News

JAFO: UKARABATI WA BARABARA MSIMBU KUANZA JUNI 11

Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Selemani Jafo, ameleta afueni kwa wakazi wa Kata ya Msimbu baada ya kutangaza kuwa ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mvua utaanza rasmi Alhamisi, Juni 11, 2026.

Dkt. Jafo alitoa tamko hilo Juni 8, 2026 wakati wa ziara maalum ya kukagua hali ya barabara hizo. Katika ziara hiyo aliambatana na Meneja wa TARURA Wilaya ya Kisarawe, Mhandisi Africano Orota, pamoja na mkandarasi kutoka kampuni ya VEDMA Investment Company Limited, iliyokabidhiwa utekelezaji wa mradi huo.

Ziara hiyo ilihusisha maeneo ya Majumba Sita, Homboza Stendi na Homboza Hospitali, ambapo mbunge huyo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi na kusikiliza changamoto zinazowakabili kutokana na ubovu wa miundombinu hiyo.
"Ninawaomba TARURA na mkandarasi kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa haraka na kwa viwango vinavyotakiwa ili wananchi wetu waweze kupata huduma bora za usafiri," alisema Dkt. Jafo.

Aidha, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa wataalamu watakaohusika na utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na ubora unaohitajika.

Dkt. Jafo pia alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa wakati kwa ajili ya ukarabati wa barabara zilizoharibiwa na mvua katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Kata ya Msimbu.
Barabara zitakazofanyiwa ukarabati ni Makamo wa Rais–Majumba Sita hadi Homboza Stendi (kilomita 4), Homboza Stendi kupitia Shule ya Msingi hadi Palaley (kilomita 6), Homboza Stendi kupitia Shule ya Sekondari hadi Msanga Zalala (kilomita 4), pamoja na Bwama kupitia Mwanzo Mgumu hadi Msanga Zalala (kilomita 6).

Kwa upande wao, wananchi wa Msimbu walionesha furaha na kumpongeza Dkt. Jafo kwa kufika kujionea changamoto zinazowakabili, huku wakiahidi kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa na kukamilika kwa mafanikio.