Breaking News

MABAHARIA WAASWA KUENDELEA KUWA MABALOZI WAZURI WA NIDHAMU, WELEDI NA UZALENDO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mhandisi Ali Said Bakar, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed, amesema lengo kuu la Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani ni kujenga uelewa kwa umma kuhusu mchango mkubwa wa kiuchumi na kijamii unaotolewa na mabaharia.

Akizungumza katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yaliyofanyika Juni 22, 2026 jijini Kigoma, Mhandisi Bakar alisema serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zinatambua mchango wa mabaharia na kutumia fursa hiyo kutoa pole kwa familia zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika shughuli mbalimbali za ubaharia.
Aidha, alisema kuwa licha ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya usafiri wa majini, bado yapo matatizo yanayowakabili mabaharia, hususan katika eneo la ajira. Alieleza kuwa baadhi yao hukumbana na mikataba duni ya ajira, ucheleweshaji wa mishahara, kupewa kazi zisizoendana na taaluma zao au kukosa ajira kabisa.

"Serikali kwa kushirikiana na waajiri inaendelea kuboresha mikataba ya ajira ili kuhakikisha mabaharia wanapata mazingira bora ya kazi, usalama na maslahi stahiki yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi," alisema.
Mhandisi Bakar pia alitoa wito kwa wamiliki wa meli na mawakala wa ajira za baharini kuongeza fursa za ajira, kuheshimu haki za mabaharia na kuzingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya ajira ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kuwa na tija zaidi.

Aidha, aliwataka mabaharia kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa nidhamu, weledi na uzalendo popote wanapotekeleza majukumu yao duniani.
"Ninawasihi mabaharia waepuke kutumiwa vibaya na watu wenye tamaa, ikiwemo kubebeshwa dawa za kulevya, kusafirisha watu kinyume cha sheria au kushiriki vitendo vingine vinavyoweza kuharibu sifa ya taifa na soko la ajira za mabaharia duniani. Dunia ya leo inahitaji mabaharia wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia," alisisitiza.

Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutambua mchango wa mabaharia katika maendeleo ya uchumi na biashara duniani pamoja na kujadili changamoto na fursa zinazokabili sekta hiyo.