Breaking News

MHE. MCHENGERWA: JINA LA RAIS SAMIA LIBEBWE KWA UBORA WA HUDUMA ORCI

Na WAF – Da r es Salaam - Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameitaka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kuhakikisha inatumia ipasavyo jengo jipya la PET-CT Scan la ‘Dr. Samia Suluhu Hassan PET Centre’ pamoja na vifaa vya kisasa vilivyowekezwa na Serikali, ili kuendana na heshima ya jina la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo hilo leo Juni 20, 2026 jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huo na ina matarajio makubwa ya kuona huduma bora na zenye viwango vya juu zikiendelea kutolewa kwa wananchi wanaohitaji matibabu ya saratani.
Amesema ameridhishwa na utendaji wa wataalamu wa ORCI ambao wameendelea kuonesha uzalendo na kujituma katika kuwahudumia wagonjwa, huku tathmini mbalimbali zikionesha kuwa ubora wa huduma unaendelea hata baada ya viongozi wa Serikali kuondoka katika taasisi hiyo.

“Wagonjwa pamoja na wataalamu wanaotumwa kufanya ukaguzi wamekuwa wakitoa mrejesho chanya kuhusu huduma zinazotolewa hapa, jambo linalodhihirisha kuwa watumishi wa ORCI wanafanya kazi zao kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya taaluma” amesema Mhe. Mchengerwa
Aidha, amesema ujenzi wa jengo la "Dr. Samia Suluhu Hassan PET Centre" pamoja na vifaa vilivyozinduliwa umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 25, uwekezaji ambao unalenga kuimarisha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Waziri Mchengerwa amesisitiza kuwa ni wajibu wa ORCI kuhakikisha uwekezaji huo mkubwa unaleta matokeo yaliyokusudiwa na kuendelea kulinda hadhi ya taasisi hiyo pamoja na jina la Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa huduma bora, salama na zenye kuleta matumaini kwa wagonjwa wa saratani nchini