Breaking News

MSTAAFU KIKWETE NA RUTO WAKUTANA OSLO FORUM 2026

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amekutana na Rais wa Kenya, William Samoei Ruto, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Amani la Oslo 2026 (Oslo Forum 2026) unaofanyika jijini Oslo nchini Norway kuanzia Juni 10 hadi 11, 2026.

Viongozi hao walionekana wakisalimiana na kufanya mazungumzo pembezoni mwa mkutano huo wa kimataifa wa kila mwaka unaowakutanisha wasuluhishi wa migogoro, viongozi wa ngazi za juu serikalini, pamoja na wataalamu wa masuala ya amani kutoka zaidi ya nchi 50 duniani.

Mwaka huu, mkutano wa Oslo Forum umebeba kaulimbiu isemayo “Gharama ya Vita, Thamani ya Amani” (The Cost of War, the Price of Peace), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhimiza mazungumzo, usuluhishi wa migogoro na ujenzi wa amani katika maeneo mbalimbali duniani.

Oslo Forum ni jukwaa muhimu la kimataifa linalotoa nafasi kwa viongozi na wadau wa amani kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto za usalama na kutafuta suluhisho la migogoro inayolikabili dunia.