VIJANA WAHIMIZWA KUTUMIA FURSA ZA KIUCHUMI, KUEPUKA VITENDO VINAVYOHATARISHA AMANI
Vijana nchini wametakiwa kujikita katika kutafuta na kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao badala ya kutumiwa na baadhi ya wanasiasa au makundi yenye maslahi binafsi kuvuruga amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Wito huo umetolewa na mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Ally Mohammad, ambaye ni mmoja wa wanufaika wa programu mbalimbali za uwezeshaji wa vijana kiuchumi, ikiwemo mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.
Akizungumza kuhusu nafasi ya vijana katika maendeleo ya Taifa, Bw. Mohammad alisema vijana wengi wamekuwa wakitumia muda mwingi katika shughuli zisizo na tija, hususan kwenye mitandao ya kijamii, badala ya kuangalia fursa zinazoweza kuwainua kiuchumi.
"Napenda kutoa rai kwa vijana wenzangu kote nchini kujikita zaidi katika kutafuta na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao. Tusitumie muda mwingi mitandaoni kushiriki mijadala yenye matusi au mambo yanayoweza kusababisha uvunjifu wa amani tuliyonayo nchini," alisema.
Aliongeza kuwa amani ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa na kwamba vijana wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya watu au makundi yanayoweza kuwashawishi kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
"Amani ikitoweka hatuna nchi nyingine ya kwenda. Ni wajibu wetu sote kuilinda na kuidumisha kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho," alisisitiza.
Aidha, alisema changamoto ya ajira si tatizo linaloikumba Tanzania pekee bali ni suala linaloikabili dunia nzima, hivyo vijana wanapaswa kuwa wabunifu kwa kutumia rasilimali na fursa zilizopo katika mazingira yao ili kujiongezea kipato na kuchangia maendeleo ya jamii.
Bw. Mohammad alihimiza vijana kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za maendeleo huku wakitunza amani, umoja na mshikamano ambao umeendelea kuwa nguzo muhimu ya maendeleo nchini




