PROF MKUMBO: SERIKALI KUENDELA KUWAIMARISHA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI KWA MITAJI NA UTAFITI
Dar es salaam - Serikali imeahidi kuendelea kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini nchini kupitia upatikanaji wa mitaji, maeneo ya uchimbaji na kuimarisha shughuli za utafiti wa kijiolojia ili kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya kupokea ripoti ya mapendekezo ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini nchini.
Profesa Mkumbo alisema serikali imeamua kutumia ushahidi wa kisayansi na matokeo ya tafiti katika kufanya maamuzi ya maendeleo ya sekta ya madini, hatua ambayo itawezesha utekelezaji wa sera na mipango yenye matokeo chanya kwa wananchi.
Alisema tayari Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta hiyo, ikiwemo kutenga asilimia 10 ya mapato yanayotokana na sekta ya madini kwa ajili ya shughuli za utafiti na maendeleo.
“Waziri wa Madini amekuwa mstari wa mbele kusukuma agenda ya kuwawezesha wachimbaji wadogo. Sasa tunaweka nguvu katika kufanya maamuzi yanayotokana na ushahidi wa kisayansi ili sekta hii iweze kuchangia zaidi ukuaji wa uchumi, ajira na kupunguza umaskini,” alisema Profesa Mkumbo.
Alieleza kuwa pamoja na mchango mkubwa wa makampuni makubwa ya uchimbaji katika kuongeza mapato ya taifa na mauzo ya nje, wachimbaji wadogo wana nafasi muhimu zaidi katika kuzalisha ajira na kupunguza umaskini kwa wananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, sekta ya madini ni miongoni mwa sekta tisa za kimageuzi zilizochaguliwa kuongoza ukuaji wa uchumi kutokana na mchango wake mkubwa katika mauzo ya bidhaa nje ya nchi, mapato ya serikali, ajira na uwezo wake wa kuchochea sekta nyingine za uchumi.
Alibainisha kuwa licha ya Mkoa wa Geita kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa dhahabu nchini, bado unakabiliwa na viwango vya juu vya umaskini, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwawezesha wachimbaji wadogo ili manufaa ya rasilimali za madini yawafikie wananchi wengi zaidi.
Profesa Mkumbo aliwataka wachimbaji wadogo kurasimisha shughuli zao kwa kusajili kampuni na vikundi vya uchimbaji ili waweze kupata fursa za kifedha, hifadhi ya jamii na masoko rasmi.
Aidha, aliwahimiza kutumia mafanikio wanayoyapata kuajiri Watanzania wengine na kuchangia maendeleo ya jamii zinazowazunguka.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkumbo alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya madini hususan wachimbaji wadogo, jambo ambalo amesema limepunguza migogoro iliyokuwa ikijitokeza kati ya wachimbaji wadogo na makampuni makubwa ya uchimbaji.
“Lengo letu si kubaki na wachimbaji wadogo milele, bali kuona wanakua na kuwa kampuni kubwa za uchimbaji zinazomilikiwa na Watanzania,” alisema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisema mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya madini yameongeza kwa kiasi kikubwa mapato ya serikali.
Alisema mwaka wa fedha 2015/2016 sekta ya madini ilikusanya takribani Sh bilioni 160 pekee, lakini baada ya marekebisho ya sheria za madini mwaka 2017, kuanzishwa kwa masoko ya madini na kuimarishwa kwa udhibiti wa biashara haramu, makusanyo yameongezeka kwa kiwango kikubwa.
“Mwaka huu wa fedha sekta ya madini imewekewa lengo la kukusanya Sh trilioni 1.5, na hadi sasa zaidi ya Sh trilioni 1.3 zimekwishakusanywa,” alisema Mavunde.
Alifafanua kuwa wachimbaji wadogo wanachangia takribani asilimia 40 ya makusanyo yote ya sekta hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto za ukosefu wa mitaji, teknolojia na taarifa sahihi za kijiolojia.
Kutokana na hali hiyo, alisema wizara imeandaa mpango maalumu wa kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili kuongeza uzalishaji na mchango wao katika uchumi wa taifa.
Dhamana ya Mikopo kwa Wachimbaji
Mavunde alisema serikali imefanya mazungumzo na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na Wizara ya Fedha kuhusu matumizi ya mfumo wa dhamana ya mikopo kupitia kampuni ya Credit Guarantee Corporation itakayoanza kazi rasmi Julai mwaka huu.
Kupitia mfumo huo, serikali itadhamini sehemu ya mikopo ya wachimbaji wadogo wanaoshindwa kutimiza masharti ya taasisi za fedha, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa kundi hilo.
Mbali na hilo, alisema serikali itaendelea kuwapatia wachimbaji wadogo maeneo rasmi ya uchimbaji na kufuta leseni za wamiliki ambao hawatekelezi masharti ya leseni zao.
Asilimia 10 kwa Utafiti wa Madini
Mavunde alisema moja ya mafanikio makubwa yaliyopatikana ni uamuzi wa Rais Samia kuridhia asilimia 10 ya mapato yanayotokana na sekta ya madini kutengwa kwa ajili ya shughuli za utafiti.
Alisema fedha hizo zitasaidia kuboresha taarifa za kijiolojia, kuongeza maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kuwasaidia wachimbaji kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.
“Fedha hizi zitatuwezesha kufanya utafiti wa kina zaidi na kuwapa wachimbaji taarifa sahihi za maeneo yenye madini badala ya kutegemea bahati,” alisema.
Tanzania Kituo Kikuu cha Biashara ya Dhahabu
Waziri Mavunde alisema serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha biashara ya dhahabu barani Afrika kwa kuimarisha mfumo wa masoko, upatikanaji wa mitaji na huduma za usafishaji wa madini.
Alieleza kuwa kwa muda mrefu wachimbaji wengi wadogo wamekuwa wakitegemea mitaji kutoka nje ya nchi, hususan Dubai, hali inayowafanya kuuza madini yao kwa wafadhili hao.
Kwa kuweka mazingira bora ya kifedha nchini, alisema serikali inalenga kuhakikisha biashara kubwa ya dhahabu inayofanyika nje ya nchi inahamia Tanzania, jambo litakaloongeza thamani ya madini na mapato ya taifa.
Mavunde alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuona wachimbaji wadogo wanakua kiuchumi na baadaye kuwa wawekezaji wakubwa wa ndani watakaomiliki kampuni kubwa za uchimbaji na kuchangia zaidi maendeleo ya taifa.









