Breaking News

SHEIKH ABDALLAH: UJANA NI NEEMA ISIYODUMU

Sheikh Abdallah Abdulqadir Al Ahdal, amewahimiza vijana kuutumia ujana wao katika kumcha Mwenyezi Mungu, kutafuta elimu, kufanya ibada na kujenga msingi imara wa maisha, pamoja na kudumisha amani, umoja na mshikamano kwani kipindi hicho ni fursa adhimu isiyodumu milele na kwamba kinatakiwa kuwa msingi wa mafanikio ya duniani na akhera.

Akitoa Khutba ya Ijumaa katika Msikiti wa Jamiul Nurul Hikma uliopo Temeke Mwembeyanga, Dar es Salaam, amesema mwanadamu hupitia hatua za utoto (udhaifu na utegemezi), ujana na uzee (ambacho pia ni kipindi cha udhaifu) huku ujana ukiwa kipindi cha nguvu na uwezo wa kutekeleza mambo makubwa. Amesisitiza kuwa nguvu hizo zinapaswa kutumika katika mema badala ya kupotezwa kwa mambo yasiyo na manufaa.

Akirejea mafundisho ya Qur'an na Hadithi za Mtume Muhammad (SAW), Sheikh Abdallah ambaye pia ni kijana, amesema Mwenyezi Mungu amewasifu vijana wema, akiwataja Vijana wa Pangoni (As-habul Kahf) waliolinda imani yao kwa kukimbia dhuluma za watawala, pamoja na Nabii Yusuf aliyekataa kufanya zinaa licha ya kushawishiwa.

Pia amemtaja mwanazuoni Ahmad ibn Hanbal aliyeanza kujifunza dini tangu utotoni kwa malezi mazuri ya mama yake, akisema mafanikio ya vijana yanahitaji malezi bora na bidii katika kutafuta elimu.

Ameikumbusha hadithi ya Mtume (SAW) isemayo: "Fanya mambo matano kabla ya matano mengine kukufikia: ujana kabla ya uzee, afya kabla ya ugonjwa, utajiri kabla ya umasikini, muda wa faragha kabla ya shughuli kukubana na maisha kabla ya kifo." Pia ameeleza hadithi nyingine inayobainisha kuwa mja hataondoka mbele ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama mpaka aulizwe kuhusu alivyotumia neema za maisha yake, ujana wake, mali yake na elimu yake.

Akihitimisha khutba hiyo, Sheikh Abdallah amewahimiza vijana wenye uwezo kufunga ndoa, akisema ndoa ni kinga dhidi ya maovu ikiwemo zinaa, huku akirejea hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) inayowataka vijana wenye uwezo kuoa ili kulinda macho na heshima zao.

Source Tbc Digital