Breaking News

SHERIA YA ULINZI WA TAARIFA YAANZA KUNG'ATA

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, Sura ya 44, pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaokiuka matakwa ya sheria hiyo.

Akizungumza leo Juni 12, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa PDPC, Dkt. Emmanuel Mkilia, amesema tume imepokea malalamiko mengi ya wananchi kuhusu matumizi ya taarifa zao binafsi bila idhini, na kwamba tayari hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Amesema zaidi ya taasisi 14,000 zinazojihusisha na ukusanyaji na matumizi ya taarifa binafsi tayari zimesajiliwa na kutambuliwa na PDPC.

Kwa sasa, tume inaendelea kufanya ukaguzi kuhakikisha taasisi hizo zinazingatia sheria, ikiwemo kuwa na sera sahihi za ulinzi wa taarifa binafsi.

Dkt. Mkilia pia ametoa muda wa siku saba za kazi kwa taasisi au watu ambao bado hawajasajiliwa kukamilisha usajili wao, kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

Kwa upande wa wananchi, mkazi wa Dodoma, Aisha Ally, amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipiga picha za wenzao katika hali zisizofaa na kuzisambaza mitandaoni, hali inayosababisha madhara makubwa ya kisaikolojia.

Amesema utekelezaji wa sheria hiyo utasaidia kukomesha vitendo hivyo.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Dativa Stephano, ambaye amesema usambazaji wa taarifa za mtu bila ridhaa unaweza kusababisha madhara makubwa, ikiwemo msongo wa mawazo na hata kujiua, akiiomba serikali kuendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria hiyo.