TANZANIA NA SINGAPORE ZAKUBALIANA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, wameeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo ya rasilimali watu kati ya nchi hizo mbili.
Wakizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu jijini Dares Salaam, Juni 9, 2026 viongozi hao walisema ziara ya kitaifa ya Mhe. Rais Tharman nchini Tanzania imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya mataifa hayo yanayoadhimisha miaka 45 ya uhusiano wa kidiplomasia.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mhe. Rais Samia alisema Tanzania inalenga kunufaika na uzoefu wa Singapore katika maendeleo ya bandari, biashara, teknolojia, elimu na ujenzi wa ujuzi kwa vijana ili kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga pamoja na mambo mengine kuwajengea vijana ujuzi ili kuwawezesha kujiajiri.
Alisema katika mazungumzo yao walikubaliana kukuza uhusiano kati ya Tanzania na Singapore ili we thabiti, imara na wenye matokeo yanayoonekana na yenye manufaa kwa nchi hizi mbili na wat wake, ambapo pia Mhe. Rais Samia aliikaribisha Singapore kufungua ubalozi wake hapa nchini.
Mheshimiwa Rais Samia pia alisema anawakaribisha Singapore kuwekeza nchini katika kilimo cha uzalishaji kupitia utaratibu wa kuzalisha nje ya nchi yaani wao waje wazalishe huku kwetu na kusafirisha nchini kwao.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Rais Tharman alisema Tanzania ina nafasi muhimu kama lango la biashara kwa Afrika Mashariki kutokana na eneo lake la kimkakati na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya usafirishajivna biashara.
Viongozi hao pia walishuhudia kusainiwa kwa hati za makubaliano ya ushirikiano katika maeneo ya maendeleo ya ujuzi, biashara, uwekezaji na ushirikiano wa masoko ya kaboni. Aidha, walikubaliana kuendeleza majadiliano kuhusu makubaliano ya biashara huria kati ya Singapore na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na ushirikiano katika sekta ya afya, hususan utafiti wa ugonjwa wa selimundu.




