Breaking News

TPBA KUZINDUA KITABU CHA FALSAFA YA SHERIA YA MAMA SAMIA JUNI12

Dar es Salaam. Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kinatarajia kuzindua kitabu maalum kiitwacho Falsafa ya Sheria ya Mama Samia (Mama Samia Doctrine of Law) Juni 12, 2026 katika Ukumbi Mpya wa Maktaba wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uzinduzi huo utaanza saa 1:30 asubuhi na unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wataalamu wa sheria, wasomi pamoja na wananchi mbalimbali.

Kwa mujibu wa TPBA, kitabu hicho kimeandaliwa kwa lengo la kuandika na kuhifadhi historia ya mageuzi makubwa yaliyofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kitabu hicho kinajadili kwa kina mageuzi yaliyofanyika katika sekta mbalimbali ikiwemo sheria, utoaji wa haki, uchumi, uwekezaji, diplomasia, utawala bora, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), elimu, afya na maendeleo ya kijamii. Aidha, kinaeleza namna mageuzi hayo yanavyohusiana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 hadi 2050.
TPBA imeeleza kuwa maandalizi ya kitabu hicho yalihusisha utafiti wa kina uliotumia takwimu, nyaraka rasmi na uchambuzi wa kitaalamu. Kabla ya kuchapishwa, kazi hiyo ilifanyiwa tathmini na uhakiki wa kitaalamu na maprofesa, watafiti pamoja na wataalamu mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha ubora wa maudhui na usahihi wa takwimu zilizotumika.

Mgeni rasmi katika hafla hiyo anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku Mlezi wa TPBA ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari, akitarajiwa kushiriki katika tukio hilo.

TPBA imewaalika Watanzania wote kushiriki katika uzinduzi huo ambao unatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kutunza kumbukumbu za mageuzi ya taifa na kutoa mwanga kuhusu safari ya Tanzania kuelekea Dira ya Maendeleo 2050.

Kaulimbiu ya kitabu hicho ni: “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia: Mageuzi, Uongozi na Dira ya Tanzania ya Kesho.”