VYOMBO VYA HABARI VYA MTANDAONI VYAONGOZA KUWASILISHA KAZI SAMIA KALAMU AWARDS 2026
Vyombo vya habari vya mtandaoni vinaongoza kwa kuwasilisha kazi za kuwania Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo za Samia Kalamu Awards (SKA) 2026, huku jumla ya kazi 624 zikiwa zimewasilishwa hadi kufikia Juni 15, 2026.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa tuzo hizo ambao ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), kazi 276 sawa na asilimia 44 ya kazi zote zilizowasilishwa zimetoka katika vyombo vya habari vya mtandaoni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa magazeti yamewasilisha kazi 178, sawa na asilimia 29 ya jumla ya kazi zilizopokelewa, huku televisheni zikiwasilisha kazi 102 (asilimia 16), redio kazi 60 (asilimia 10) na majarida kazi nane pekee, sawa na asilimia moja ya kazi zote zilizowasilishwa.
Kwa upande wa makundi ya tuzo, kazi 20 sawa na asilimia 4.8 zimewasilishwa katika kundi la tuzo za vyombo vya habari, kazi 25 sawa na asilimia 4.0 katika kundi la tuzo maalum za kitaifa, huku kazi 569 sawa na asilimia 91.2 zikiwasilishwa katika makundi ya tuzo za kisekta.
Waandaaji wa tuzo hizo wamesema mwitikio huo mkubwa unaashiria kuongezeka kwa matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika uzalishaji na usambazaji wa habari za maendeleo nchini. Aidha, umeonesha dhamira ya waandishi wa habari kuendelea kuelimisha, kuhabarisha na kuhamasisha jamii kuhusu masuala ya maendeleo ya taifa.
Wamewapongeza waandishi wa habari na vyombo vya habari ambavyo tayari vimewasilisha kazi zao, huku wakiwahimiza wale ambao bado hawajakamilisha mchakato huo kutumia muda uliosalia kuwasilisha kazi zao kabla ya kufungwa rasmi kwa dirisha la maombi.
Taarifa hiyo imekumbusha kuwa dirisha la kupokea kazi za kuwania Samia Kalamu Awards 2026 litafungwa Juni 30, 2026 saa 5:59 usiku. Kazi zinazostahili kushindanishwa ni zile zilizochapishwa au kurushwa kati ya Julai 1, 2025 na Juni 30, 2026.
Samia Kalamu Awards ni jukwaa la kitaifa lililoanzishwa kwa lengo la kutambua, kuthamini na kuhamasisha ubora, weledi na ubunifu katika uandishi wa habari za maendeleo nchini, kupitia kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo.”




