ASANTE AFRIKA GROUP YAADHIMISHA MIAKA SABA, YAAHIDI KUONGEZA HUDUMA NA KUSAIDIA SEKTA ZA ELIMU NA AFYA
Dar es Salaam: Asante Afrika Group of Companies kupitia kampuni yake tanzu ya Asante Motors Limited imetangaza kuadhimisha miaka saba tangu kuanzishwa kwake, huku ikiahidi kuendelea kuboresha huduma, kupanua uwekezaji na kuchangia maendeleo ya jamii kupitia sekta za elimu, afya na usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Asante Afrika Group of Companies, Elisante Ibrahim, alisema mafanikio ya kampuni hiyo yamejengwa katika misingi ya uaminifu, ubora wa huduma na kujibu mahitaji ya Watanzania.
Alisema kampuni imejikita katika kuagiza bidhaa na vifaa kutoka masoko ya kimataifa kwa viwango vinavyokubalika duniani, huku ikitoa huduma kuanzia ushauri wa kitaalamu, uchaguzi wa bidhaa, ununuzi, usafirishaji hadi kukabidhi bidhaa kwa mteja.
Elisante alisema kuelekea maadhimisho ya miaka saba, kampuni imeanzisha mpango maalumu wa kusaidia sekta za elimu na afya kwa kuondoa ada za uagizaji wa magari na vifaa kwa shule, hospitali na vituo vya afya ili kupunguza gharama za huduma.
Alisema kampuni pia itatoa msaada wa vifaa vinavyohitajika katika huduma za mama na mtoto pamoja na watoto njiti, baada ya kufanya mashauriano na wadau wa sekta ya afya kuhusu maeneo yenye uhitaji mkubwa
Aidha, alisema kampuni itashirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vya habari kutoa elimu ya usalama barabarani kwa lengo la kupunguza ajali na kulinda nguvu kazi ya taifa.
Katika hafla hiyo, Asante Motors Limited ilimtangaza rasmi Paul Stephen Mnyoro maarufu kama Mr Paul kuwa balozi wa chapa (Brand Ambassador), akitarajiwa kushiriki kutangaza huduma za kampuni, kuimarisha chapa yake, kuhamasisha vijana kuhusu fursa mbalimbali pamoja na kushiriki kampeni za kijamii.
Kwa upande wake, Afisa masoko na Uhusiano na Masoko wa Asante Motors Limited, Yusuph Yusuph alisema kampuni inatoa huduma mbalimbali zinazolenga kurahisisha umiliki wa magari kwa Watanzania.
Alizitaja huduma hizo kuwa ni kifurushi cha kuagiza magari kutoka nje ya nchi, kifurushi cha mikopo ya magari kinachotekelezwa kwa kushirikiana na taasisi za fedha, pamoja na huduma ya "dunduliza gari" inayowawezesha wateja kuweka akiba kidogo kidogo hadi kufikia gharama za kuagiza au kununua gari.
Alisema kampuni pia inatoa ushauri wa kitaalamu kwa wateja kuhusu uchaguzi wa magari yanayofaa, matumizi sahihi ya mafuta na vipuri pamoja na namna bora ya kutunza magari baada ya ununuzi.
Yusuph aliongeza kuwa kampuni imeanzisha kifurushi maalumu cha elimu na afya kinacholenga kusaidia wamiliki wa shule na hospitali kuagiza magari na vifaa kwa gharama nafuu, hatua ambayo alisema itachangia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kuhusu mikopo ya magari, alisema kampuni inashirikiana na taasisi mbalimbali za kifedha zinazotoa mikopo yenye riba pamoja na taasisi zinazotoa huduma za kifedha zinazozingatia misingi ya Kiislamu isiyo na riba, ili kuwapa wateja uchaguzi kulingana na mahitaji yao.
Naye balozi mpya wa Asante Motors Limited, Paul Stephen Mnyoro (Mr Paul), aliishukuru kampuni kwa kumuamini na kusema atatumia nafasi hiyo kuhamasisha Watanzania kutumia huduma za kampuni pamoja na kushiriki kampeni za elimu, afya na maendeleo ya jamii.
Alisema mafanikio ya biashara yanapaswa kwenda sambamba na maendeleo ya jamii, hivyo ataendelea kuhamasisha wananchi kutumia fursa zinazotolewa na Asante Motors Limited kwa manufaa yao na ya taifa.






