Breaking News

CCM NA ACT WAZALENDO WATIA SAINI TAMKO LA MARIDHIANO ZANZIBAR

Zanzibar – Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha ACT Wazalendo vimetia saini Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa lenye lengo la kuendeleza mazungumzo na kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa zilizojitokeza baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 upande wa Zanzibar.

Tamko hilo, lililosainiwa kwa niaba ya CCM na Mohammed Said Mohammed na kwa niaba ya ACT Wazalendo na Omar Ali Shehe, linaweka msingi wa kuimarisha umoja wa kitaifa, amani, utulivu, demokrasia na utawala bora kupitia mchakato wa mazungumzo unaohusisha wadau mbalimbali.

Pande hizo mbili zimesema zitaendelea kushirikiana katika kujenga maridhiano ya kweli ili kurejesha imani ya wananchi pamoja na wadau wa uchumi, biashara na uwekezaji, huku zikiahidi kuimarisha taasisi za kidemokrasia, utawala wa sheria na kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na wenye uwazi.

Tamko hilo limeeleza kuwa mchakato wa maridhiano utakuwa shirikishi kwa kuwahusisha wananchi, vyama vya siasa, asasi za kiraia na makundi mbalimbali ya kijamii, huku ukiongozwa na misingi ya ukweli, uadilifu na kuweka mbele maslahi ya Zanzibar badala ya maslahi ya vyama au watu binafsi.

Aidha, pande hizo zimekubaliana kuunda Kamati ya Pamoja itakayopendekeza mfumo, taratibu na hatua za utekelezaji wa ajenda walizokubaliana. Baada ya mapendekezo hayo, chombo maalumu kitaundwa kwa mujibu wa sheria ili kusimamia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Kwa mujibu wa tamko hilo, utekelezaji wa makubaliano utaanza mara moja baada ya kutolewa kwa tamko hilo, huku wananchi wa Zanzibar wakitakiwa kuunga mkono mchakato huo kwa lengo la kufungua ukurasa mpya wa maridhiano na maendeleo ya nchi.

Mchakato huo ulianza kufuatia ushauri wa Marais Wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohammed Shein, baada ya kutokea kutokubaliana kati ya CCM na ACT Wazalendo kuhusu uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kufuatia malalamiko yaliyoibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa tamko hilo, jumla ya vikao tisa vya viongozi na vikao viwili vya kamati ndogo vilifanyika kati ya Novemba 9, 2025 na Mei 25, 2026. Vikao vya mwisho vilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa Othman Masoud Othman, Mwenyekiti Mstaafu wa ACT Wazalendo Juma Duni Haji pamoja na Marais Wastaafu waliokuwa wasimamizi wa mazungumzo hayo.

Pande hizo zimesisitiza kuwa zitasimamia mchakato huo kwa dhamira ya dhati, zikitanguliza maslahi ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kupata suluhisho la kudumu la changamoto za kisiasa, kijamii na kiutawala.