Breaking News

KOM FOOD PRODUCTS YAJIVUNIA MAPOKEZI MAKUBWA SABASABA, YATANGAZA FURSA KWA WAKULIMA NA WAJASIRIAMALI

Na Mwandishi Wetu - Kampuni ya KOM Food Products ya Halmashauri ya Shinyanga imesema imepokelewa kwa mwitikio mkubwa katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), huku ikitangaza kuanza kusambaza bidhaa zake rasmi katika soko la Dar es Salaam na kutoa fursa kwa mawakala pamoja na wakulima.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkuu wa Masoko na Mauzo wa KOM Food Products, Innocent Mafuru, alisema kampuni hiyo imeingia kwa mara ya kwanza katika soko la Dar es Salaam kupitia maonesho hayo na imevutiwa na mapokezi makubwa kutoka kwa wateja.

Alisema kampuni hiyo huzalisha mchele wa viwango mbalimbali vya ubora (Grade One, Grade Two na Grade Three), unga pamoja na vyakula vya mifugo, huku mchele ukiwa umezingatia viwango vya ubora vinavyokubalika sokoni.

Mafuru alisema bidhaa za kampuni hiyo sasa zinapatikana katika ofisi zao zilizopo Mtaa wa Mkwepu, jengo la Diplomat House, pamoja na maduka makubwa na supermarket mbalimbali kuanzia Kigamboni, Tabata hadi Mbezi Beach. Aliongeza kuwa mchele huo umefungwa katika vifungashio vya kilo 1, kilo 5 na kilo 25, huku bei ya maonesho ikianzia Sh3,000.

Aidha, alisema maonesho ya Sabasaba yameiwezesha kampuni hiyo kukutana na wafanyabiashara kutoka Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, hatua inayofungua fursa ya kupanua soko la bidhaa zake ndani na nje ya Tanzania.

Kuhusu kuwawezesha wananchi kiuchumi, Mafuru alisema kampuni imenunua mpunga kwa wingi kutoka kwa wakulima wa Kahama na maeneo jirani na kiwanda chake, jambo ambalo limewapa wakulima uhakika wa soko na bei nzuri za mazao yao.

Pia aliwataka wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kujitokeza kuwa mawakala wa usambazaji wa bidhaa za KOM Food Products nchini, akisema kampuni imeweka masharti nafuu yatakayowawezesha kufanya biashara na kuongeza kipato chao.

Alisema hatua hiyo inaunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha Watanzania kiuchumi kupitia uzalishaji, biashara na ujasiriamali.